UNICEF: Watoto 8 wameuawa katika mapigano Yemen
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i68162-unicef_watoto_8_wameuawa_katika_mapigano_yemen
Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuwahudumia Watoto (UNICEF) limesema watoto 8 wameuawa katika mapigano nchini Yemen huku wengine 33 wakijeruhiwa katika mwezi huu wa MachI huku Saudi Arabia na washirika wake wakiendeleza mashambulio na mzingiro dhidi ya nchi hiyo masikini zaidi katika Bara Arabu.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Mar 21, 2021 22:01 UTC
  • UNICEF: Watoto 8 wameuawa katika mapigano Yemen

Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuwahudumia Watoto (UNICEF) limesema watoto 8 wameuawa katika mapigano nchini Yemen huku wengine 33 wakijeruhiwa katika mwezi huu wa MachI huku Saudi Arabia na washirika wake wakiendeleza mashambulio na mzingiro dhidi ya nchi hiyo masikini zaidi katika Bara Arabu.

Kwa mujibu wa taarifa ya Jumapili ya  televisheni ya Rousiya al Youm, Philippe Duamelle, mjumbe ya UNICEF nchini Yemen. amelaani kushadidi mapigano baina ya wapiganaji watiifu kwa rais wa Yemen aliyejiuzulu Abdul Rabuh Mansour Hadi na vikosi vya Jeshi la Yemen katika maeneo kadhaa hasa katika mikoa ya Taizz na Al Hudaydah.

Afisa huyo wa UNICEF amesema watoto wa Yemen na familia zao ndio waathirika wakubwa zaidi wa mapigano nchini humo.

Aidha Duamelle amesema katika mashambulizi ya hivi karibuni shule na hospitali zimelengwa kwa mabomu katika mkoa wa Taizz  na hali kadhalika watoto kadhaa pia wamelengwa katika mapigano mkoani Maarib.

Kufuatia mafanikio ya hivi karibuni ya Jeshi la Yemen katika mapigano na mamluki wa Saudia mkoani Maarib na pia mafanikio makubwa ya jeshi hilo katika kushambulia maeneo ya ndani kabisa ya Saudia Arabia ili kulipiza kisasi, ndege za kivita za Saudia zimeshambulia maeneo kadhaa ya raia nchini Yemen.

Utawala dhalimu wa Saudia ulianzisha mashambulizi dhidi ya Yemen mnamo Machi 2015 kwa lengo la kuiondoa madarakani Harakati ya Ansarullah na kumrejesha madarakani kibaraka wake, Abdrabbuh Mansour Hadi, rais wa zamani wa nchi hiyo aliyejiuzulu na kukimbilia Riyadh.

Watoto ni waathirika wakubwa wa vita vya Saudia dhidi ya Yemen

Hata hivyo hadi sasa Saudia na washirika wake wameshindwa kufikia malengo yao kutokana na kusimama kidete wananchi wa Yemen wakiongozwa na Harakati ya Ansarullah. Harakati hiyo imekuwa ikitekeleza mashambulizi ya kulipiza kisasi ndani ya ardhi ya Saudi Arabia ambapo imelenga mara kadhaa vituo vya kusafisha mafuta na pia viwanja vya ndege vinavyotumiwa na jeshi vamizi la utawala huo wa kifalme.

Mwezi Disemba mwaka jana,  Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu (OCHA) ilitangaza kuwa vita vya Saudi Arabia dhidi ya Yemen vimepelekea zaidi ya watu 233,000 kupoteza maisha katika kipindi cha miaka sita iliyopita.