Saudia yamtishia kifo Ripota wa UN kwa kuchunguza mauaji ya Khashoggi
Ripota Maalumu wa Umoja wa Mataifa amefichua kuwa, utawala wa Saudi Arabia umemtishia kumua kutokana na kufuatilia kwake mauaji ya mwandishi mkosoaji, Jamal Khashoggi.
Ripoti ya jana Jumanne ya shirika la habari la IRNA imemnukuu Bi Agnes Calamard akisema hayo katika mahojiano na gazeti la The Guardian na huku akitoa ushahidi kuhusu matamshi ya wafanyakazi wenzake, amesema, mwezi Januari 2020, maafisa wa utawala wa Saudia walikutana na maafisa wa taasisi yake mjini Geneva Uswisi, wakatoa tuhuma zisizo na msingi na wakamtishia kumuua kutokana na kufuatilia kwake mauaji ya Jamal Khashoggi.
Ripota huyo maalumu wa Umoja wa Mataifa amesema, maafisa hao wa ngazi za juu wa watawala wa Saudi Arabia walimtuhumu kuwa amepewa fedha na serikali ya Qatar ili aihusishe serikali ya Saudia na mauaji hayo.
Ikumbukwe kuwa, siku chache zilizopita, mrithi wa kiti cha ufalme wa Saudi Arabia ameitwa mahakamani kujibu mashtaka yanayomkabili kuhusiana na mauaji ya mwandishi mkosoaji, Jamal Khashoggi.
Kwa mujibu wa shirika la habari la ISNA, Bi Hatice Cengiz, mchumba wa Jamal Khashoggi, mwandishi aliyekuwa akiukosoa utawala wa hivi sasa wa Saudi Arabia, amefungua mashtaka mahakamani dhidi ya mrithi wa kiti cha ufalme wa nchi hiyo, Mohammad bin Salman na mahakama hiyo ya nchini Marekani imemtaka Bin Salman afikishwe mbele ya mahakama hiyo kujibu mashtaka yanayomkabili.
Bin Salman ameshtakiwa kwa makosa ya kumteka nyara na kumuua Jamal Khashoggi. Makosa mengine ni kumtesa na kumuua kinyama na kikatili mno Jamal Khashoggi, unyama ambao umeishitua dunia nzima.
Bin Salman anatuhumiwa pia kujaribu kunyamazisha sauti ya kupigania mabadiliko na demokrasia katika nchi za Kiarabu, kupitia jinai yake hiyo dhidi ya mwandishi huyo mkazi wa Marekani, Jamal Khashoggi. Hivi sasa kuna mawakili watatu wanaomwakilisha mrithi wa kiti cha ufalme wa Saudi Arabia katika kesi hiyo. Hadi inatangazwa habari hii, viongozi wa Saudi Arabia walikuwa wamekaa kimya bila ya kusema chochote kuhusu kuitwa mahakamani mrithi wa kiti cha ufalme wa nchi hiyo.