Kamanda Mkuu wa muungano vamizi wa Saudia aangamizwa Ma'rib Yemen
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i68360-kamanda_mkuu_wa_muungano_vamizi_wa_saudia_aangamizwa_ma'rib_yemen
Duru mbalimbali za Yemen zimetangaza habari ya kuangamizwa mmoja wa makamanda wakuu wa muungano vamizi wa Saudi Arabia katika mkoa wa Ma'rib nchini Yemen.
(last modified 2026-08-14T10:24:44+00:00 )
Mar 27, 2021 07:19 UTC
  • Kamanda Mkuu wa muungano vamizi wa Saudia aangamizwa Ma'rib Yemen

Duru mbalimbali za Yemen zimetangaza habari ya kuangamizwa mmoja wa makamanda wakuu wa muungano vamizi wa Saudi Arabia katika mkoa wa Ma'rib nchini Yemen.

Mtandao wa "Akhbar al Yamani" umeripoti habari hiyo na kuongeza kuwa, Amin al Waili, kamanda mkuu wa Eneo la Sita la Kijeshi la la muungano vamizi wa Saudia aliangamizwa jana usiku katika eneo la operesheni za kijeshi la Ma'rib, kwenye mapigano makali baina ya jeshi na vikosi vya kujitolea vya wananchi wa Yemen na mamluki na askari vamizi wanaoongozwa na Saudi Arabia.

Taarifa hiyo imesema, mbali na kamanda huyo mkuu wa jeshi la muungano vamizi wa Saudia, mamluki wengine kadhaa nao wameangamizwa katika mapigano hayo.

Habari nyingine zinasema kuwa, ndege za kivita za muungano vamizi wa Saudia zimefanya mashambulizi 12 katika maeneo ya Medghal na Sirwah katika mkoa wa Ma'rib.

Saudia na magenge yake wanafanya jinai zisizona kifani nchini Yemen

 

Kwa siku kadhaa mtawalia, ndege za muungano vamizi wa Saudia zimekuwa zikifanya mashambulio ya kikatili kwenye maeneo mbalimbali ya Yemen kutokana na jeshi na vikosi vya kujitolea vya nchi hiyo kuzidi kusonga mbele katika ukombozi wa mkoa wa Ma'rib wenye utajiri mkubwa wa mafuta.

Vita vya Yemen vimeshaingia katika mwaka wake wa 7. Tarehe 26 Machi 2015, Saudi Arabia kwa msaada wa Marekani, utawala wa Kizayuni wa Israel, Umoja wa Falme za Kiarabu (Imarati) na baadhi ya nchi za Ulaya na Kiarabu kama Uingereza na Sudan, ilianzisha mashambulizi ya kivamizi ya pande zote dhidi ya taifa maskini la Kiarabu na Kiislamu la Yemen.

Wavamizi hao walikuwa na ndoto ya kuvimaliza vita hivyo katika kipindi cha wiki chache tu. Hata hivyo huu ni mwaka wa 7 na kadiri siku zinavyopita, ndivyo wananchi wa Yemen wanavyozidi kuwa imara katika muqawama na kujihami kwao kishujaa.