Asarullah: Inabidi vita visimamishwe kwanza kabla ya kuanza mazungumzo
Mjumbe wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Ansarullah ya Yemen amesisitiza kuwa, inabidi muungano wa Saudi Arabia ukomeshe kwanza mashambulizi yake na kuizingira Yemen kabla ya kuanza mazungumzo yoyote yale.
Televisheni ya al Jazeera ya Qatar imemnukuu Mohammed al Bukhaiti, akisema kuwa, mazungumzo yoyote yale yatategemea kukomesha Saudia na muungano wake, mashambulizi dhidi ya Yemen na kuizingira nchi hiyo.
Vile vile amesema, Ansarullah haitoacha kuyapiga kwa makombora maeneo mbalimbali ya Saudi Arabia maadamu wavamizi hao wanaendelea kuwashambulia wananchi wa Yemen.
Amesema, kusimamishwa vita nchini Yemen ni kwa manufaa ya nchi zote za eneo hili hasa kwa kuzingatia kwamba sasa hivi mlingano wa nguvu ni kwa manufaa ya wanamuqawama wa Yemen na ni kwa madhara ya wavamizi wa nchi hiyo.
Afisa huyo mwandamizi wa harakati ya Ansarullah ya Yemen pia amesema, Marekani ni adui wa umma wa Kiislamu na umma wa Kiarabu na kwa vile mazungumzo na usimamishaji vita wa huko nyuma haukuleta matunda yoyote, sasa hivi Wayemen wanasubiri hatua za kivitendo za kukomesha mashambulizi na kuzingirwa nchi yao.
Vita vya Yemen vimeshaingia katika mwaka wake wa 7. Tarehe 26 Machi 2015, Saudi Arabia kwa msaada wa Marekani, utawala wa Kizayuni wa Israel, Umoja wa Falme za Kiarabu (Imarati) na baadhi ya nchi za Ulaya na Kiarabu kama Uingereza na Sudan, ilianzisha mashambulizi ya kivamizi ya pande zote dhidi ya taifa maskini la Kiarabu na Kiislamu la Yemen.
Wavamizi hao walikuwa na ndoto ya kuvimaliza vita hivyo katika kipindi cha wiki chache tu. Hata hivyo huu ni mwaka wa 7 na kadiri siku zinavyopita, ndivyo wananchi wa Yemen wanavyozidi kuwa imara katika muqawama na kujihami kwao kishujaa.