Kupungua akiba ya fedha za kigeni ya Saudi Arabia
Imepita miaka 6 sasa tangu Mfalme Salman bin Abdulaziz Aal Saud aliposhika madaraka nchini Saudi Arabia na mbali na kufeli kukubwa katika siasa za nje, akiba ya fedha za kigeni ya nchi hiyo pia imepungua sana na kufikia kiwango cha chini zaidi katika mwongo mmoja uliopita.
Mfalme Salman Bin Abdulaziz alishika madaraka ya nchi Januari mwaka 2015 baada ya kufariki dunia kaka yake, Abdullah. Katika kipindi cha miaka 6 iliyopita Saudia imeshuhudia mporomoko endelevu hususan katika sekta ya uchumi na nafasi yake ya kikanda. Kabla ya Mfalme Salman kushika madaraka, Saudi Arabia haikuwa ikikabiliwa na nakisi ya bajeti; suala ambalo limekuwa tatizo sugu la nchi hiyo katika miaka ya karibuni.
Mwaka jana wa 2020 serikali ya Riyadh ilikabiliwa na nakisi ya bajeti ya dola bilioni 79. Mwezi Februari mwaka huu pia akiba ya fedha za kigeni ya Saudia ilipungua sana na kufikia kiwango cha chini kabisa katika muongo wa karibuni. Ripoti ya Benki Kuu ya Saudia inaonyesha kuwa, akiba ya fedha za kigeni ya nchi hiyo mwezi Februari ilipungua kwa dola bilioni 8.77 na kufikia dola bilioni 441.3 kutoka dola bilioni 450.1. Punguo hilo la akiba ya fedha za kigeni ya Saudi Arabia halijawahi kushuhudiwa katika kipindi cha miaka 10 iliyopita.
Utendaji mbaya wa serikali ya Mfalme Salman haukuishia katika sekta ya uchumi bali Saudi Arabia imefeli pia katika masuala ya siasa za nje. Kushika madaraka Mfalme Salman na mwanaye, Muhammad kuliandamana na kuanza vita vya nchi hiyo dhidi ya taifa la Yemen, nchi ambayo ndiyo maskini zaidi katika eneo la Magharibi mwa Asia. Imepita miaka sita sasa tangu vita hivyo vianzishwe lakini hadi sasa hakuna ishara yoyote ya kupata ushindi; na zaidi, Saudia na waitifaki wake wamepata vipigo na hasara kubwa zaidi kadiri miaka inavyosonga mbele. Kutokana na hali hiyo Riyadh na waitifaki wake wa kimagharibi na Umoja wa Mataifa wameanzisha mikakati ya kutaka kuikoa Saudia Arabia katika kinamasi cha Yemen na kupungua hasara za nchi hiyo. Kimsingi moja kati ya sababu kuu za mporomoko wa kiuchumi wa Saudi Arabia na kupungua kwa akiba ya fedha za kigeni ya nchi hiyo ni kurefuka vita vya watawala wa Riyadh huko Yemen. Mwanzoni mwa vita hivyo akiba ya fedha za kigeni ya Saudia ilikuwa karibu dola bilioni 700 na hivi sasa imepungua na kufikia dola bilioni 441.
Suala jingine ni kwamba katika ushindani wao dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Aal Saud wakishirikiana na Marekani inayoshindana na Russia, walitumia fimbo ya kupunguza bei ya mafuta kwa shabaha ya kutoa pigo dhidi ya uchumi wa Tehran na Moscow. Japokuwa mafuta ya petroli na pato linalotokana na bidhaa hiyo ni suala la ndani ya nchi, lakini Saudia ilitumiaji mafuta kwa shabaha ya kutoa dhuruba na pigo dhidi ya Iran katika siasa za kigeni na suala hilo linahesabiwa kuwa ni mfano mwingine wa kufeli siasa nje za mfalme Salman bin Abdulaziz. Sasa Iran na Russia zimevuka salama athari mbaya za kupungua kwa bei ya mafuta, na chumi za nchi mbili hizo zimeendelea kusimama ngangari huku kiwango cha pato la mafuta la Saudia kikipungua na kushuka chini.

Mbali na hayo Mfalme Salman na mwanaye, Muhammad ambao walielewa vyema kwamba nguzo za utawala wao ni dhaifu ndani ya kizazi cha ukoo wa Aal Saud, waliamua kutafuta himaya zaidi kutoka Marekani na nchi kadhaa za Ulaya kwa shabaha ya kubakia madarakani na kuweza kuhimili vishindo katika ushindani wa kikanda na kieneo. Nchi hizo za Magharibi ambazo pia zimekuwa zikikodolea macho dola za Wasaudia, zilifungamanisha himaya yao kwa Riyadh na suala la manunuzi ya silaha za mabilioni ya dola kutoka Magharibi. Sifa bora zaidi inayoweza kutumiwa kwa ajili ya keleza hali ya Saudi Arabia katika kadhia hii ni ile iliyojatwa na Rais wa zamani wa Marekani, Donald Trump aliyeifananisha nchi hiyo na "gombe linalokamuliwa maziwa."
Hivi sasa na baada ya kushika madaraka serikali mpya huko Marekani, uhusiano wa Riyadh na Washington umefanyiwa marekebisho baada ya Joe Biden kusitisha hiyama isiyo na mpaka ya Washington kwa watawala wa Aal Saud. Suala hilo pia limekuwa sababu ya kuendelea kupungua akiba ya fedha za kigeni ya Saudia, kuongezeka matatizo ya kiuchumi na kufeli zaidi siasa za kigeni za Mfalme Salman bin Abdulaziz.