"Muungano wa Saudia unatafuta njia ya kujiondoa kwenye kinamasi cha Yemen"
Waziri wa Ulinzi wa Serikali ya Uokovu wa Kitaifa wa Yemen amesema muungano vamizi wa kijeshi unaoongozwa na Saudi Arabia unatapatapa na hivi sasa umeanza kutafuta njia ya kujiondoa kwenye kinamasi cha vita dhidi ya Wayemen.
Meja Jenerali Muhammad Nasser al-Atifi amesema hayo katika mahojiano na kanali ya televisheni ya al-Masira inayorusha matangazo yake kwa lugha ya Kiarabu na kuongeza kuwa, "nchi wanachama wa muungano vamizi hivi sasa zinapitia wakati mgumu, na sasa zimeanza kutafuta njia ya kuondoka Yemen."
Ameeleza bayana kuwa, muungano huo vamizi wa Saudia hautaki kusalimu amri na kukiri kuwa umeshindwa katika vita vya Yemen ukihofia kuwa hatua hiyo itazikasirisha serikali za Washington, London, Paris na Tel Aviv.
Meja Jenerali al-Atifi amesema hata waitifaki wa Riyadh walioiburuza Saudia katika vita hivyo wameanza kutafuta njia za kujivua lawama kwa lengo la kujisafisha.
Waziri huyo wa Ulinzi wa Serikali ya Uokovu wa Kitaifa wa Yemen amesisitiza kuwa, wavamizi hao hawatapa kingine ghairi ya mashambulio ya ulipizaji kisasi hadi pale watakapoamua kusimamisha hujuma, mzingiro na uvamizi dhidi ya taifa la Yemen.
Haya yanajiri siku chache baada ya vikosi vya jeshi la Yemen kushambuliwa vituo nyeti na hasasi vya Saudi Arabia katika mji mkuu Riyadh kwa kutumia ndege zisizo na rubani (drone).