Bahrain yaendelea kushuhudia maandamano ya kutaka kuachiliwa wafungwa wa kisiasa
Wananchi wa Bahrain wameendelea kuandamana wakiutaka utawala wa kiimla wa nchi hiyo kuwaachilia huru wafungwa wa kisiasa wa nchi hiyo.
Familia za wafungwa wa kisiasa wiki hii zimefanya maandamanano mtawalia ambapo sambamba na kulalamikia mazingira mabaya wanayokabiliwa nayo ndugu zao katika magereza ya Bahrain wameutaka utawala wa Manama kuwaachilia huru wafungwa hao wa kisiasa.
Sambamba na maandamano hayo, asasi za kieneo na kimataifa za kutetea haki za binadamu zimetoa taarifa kwa nyakati tofauti zikilalamkikia ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu huko nchini Bahrain.
Ripoti mbalimbali zinaonyesha kuwa, wafungwa wanaoshikiliwa katika magereza ya nchi hiyo ambao akthari yao ni wapinzani wa utawala wa Manama wanakabiliwa na mazingira mabaya ya kiafya.
Wasiwasi wa kushadidi hali mbaya ya kiafya katika magereza hayo umeongezeka baada ya hivi karibuni kuripotiwa kwamba, idadi ya wafungwa walioambukizwa virusi vya corona imeongezeka katika magereza ya Bahrain na kwamba, mamlaka husika hazilipi umuhimu suala hilo.
Tangu Februari 14, 2011, Bahrain imekuwa uwanja wa maandamano na mikusanyiko ya upinzani ya wananchi dhidi ya utawala wa kifamilia wa Aal Khalifa.
Katika kipindi cha takriban miaka minane sasa, utawala huo wa kiimla umewakamata na kuwaweka kizuizini zaidi ya raia 11,000 kwa tuhuma bandia. Hadi sasa raia kadhaa wameshanyongwa na wengine wengi wamevuliwa uraia au kuhamishwa nchini humo.
Wanachodai wananchi wa Bahrain ni kuweko mageuzi ya kimsingi katika mfumo wa uongozi nchini humo na kuweko demokrasia ya kweli.