Aprili pekee, Wapalestina 270 wamekamatwa na kuhamishwa baada kubomolewa nyumba zao
Katika mwezi mmoja tu uliopita wa Aprili, askari wa utawala haramu wa Kizayuni wa Israel wameshadidisha hujuma na mashambulio katika mji wa Baitul Muqaddas (Jerusalem) na msikiti mtukufu wa Al Aqsa; na katika kipindi hicho wamewakamata na kuwahamisha katika nyumba zao Wapalestina zaidi ya 270.
Kanali ya habari ya Meidanul-Quds imeripoti kuwa, katika mwezi huu mtukufu wa Ramadhani na tangu siku 12 zilizopita, Wazayuni wamevamia eneo la Babul-a'muud na maeneo ya kandokando ya msikiti wa Al Aqsa na kuwashambulia Wapalestina walio katika hali ya Saumu kwa mabomu ya kutoa machozi, sambamba na kuwatusi na kuwapiga.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, walowezi zaidi ya 3,400 wa Kizayuni wamevamia msikiti wa Al Aqsa na lango la Babul-a'muud na kwamba hujuma zao zimeshtadi hasa katika mwezi huu wa Ramadhani.
Wapalestina wapatao 420 waliokuwa wamefunga wamejeruhiwa na makumi ya wengine wamekamatwa katika hujuma iliyofanywa na askari wa utawala haramu wa Israel wakishirikiana na walowezi wa Kizayuni dhidi ya eneo la Babul-a'muud.
Baada ya Wazayuni kuwakamata Wapalestina hao, wamewahamisha kwa nguvu katika mji huo wa Quds na kuwabomolea nyumba zao.
Wakati huohuo makumi ya Wapalestina wa eneo la Sheikh Jarrah katika mji wa Baitul Muqaddas wanakabiliwa na hatari ya kuhamishwa katika nyumba zao ili kuhakikisha eneo hilo linakaliwa na walowezi watupu wa Kizayuni.
Tayari mahakama ya utawala wa Kizayuni katika mji wa Quds, imeshatoa hukumu ya kuzitaka familia zisizopungua sita za Wapalestina zihakikishe kuwa ifikapo leo Jumapili ziwe zimeshahama katika nyumba zao ambazo wameishi ndani yake vizazi kadhaa.
Mahakama hiyohiyo imezitaka familia nyingine saba za Wapalestina ziwe zimesha hama katika nyumba zao ifikapo Agosti mosi mwaka huu. Jumla ya watu 58 wakiwemo watoto 17 watahamishwa kwa nguvu katika nyumba zao ili maeneo yao yaporwe na kukaliwa na walowezi wa Kizayuni.../