Makumi ya maelefu ya Wapalestina washiriki Swala ya Ijumaa Al Aqsa
Makumi ya maelfu ya Wapalestina wameshiriki katika Swala ya Ijumaa jana katika Msikiti wa Al Aqsa pamoja na kuwepo vizingiti vilivyowekwa na utawala wa Kizayuni wa Israel.
Vyombo vya habari vimeripoti kuwa maelfu ya Wapalestina jana waliweza kuswali Al Aqsa pamoja na kuwepo taharuki mjini Quds (Jerusalem) ambapo wanajeshi wa utawala katili wa Israel wamekuwa wakiwashambulia. Kwa mujibu wa taarifa Wapalestina kutoka maeneo mbali mbali ya Ukingo wa Magharibi walifika katika msikiti wa Al Aqsa ambapo walipiga nara za kulaani hujuma za utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Ghaza na Quds Tukufu.
Wanamgambo Wazayuni walikabiliana na vijana wa Kipalestina ambao walikuwa wakiingia katika Msikiti wa Al Aqsa.
Katika hotuba, yake, Imamu wa Al Aqsa Sheikh Ekrima Sabri amesema utawala wa Kizayuni unapaswa kusitisha ukaliaji wake mabavu wa Msikiti wa Al Aqsa huku akitoa wito kwa Wapalestina kuhakikisha kuwa wanaondoa mzingiro dhidi ya mji wa Quds na Ukanda wa Ghaza.
Siku ya Alhamisi pia Wapalestina karibu laki moja walishiriki katika Swala ya Idul Fitr katika Msikiti wa al Aqsa ambao ni Kibla cha Kwanza cha Waislamu katika mji wa Quds licha ya sheria kali zilizowekwa na utawala wa Kizayuni wa Israel ambao katika kipindi cha siku chache umeshuhudia wanajeshi wa utawala katili wa Isreal wakiwashambulia kwa mabomu Waislamu waliokuwa wanaswali ndani ya msikiti huo.
Ukatili wa wanajeshi wa Israel umeongezeka sana katika mwezi wa Ramadhani wa mwaka huu, na utawala wa Kizayuni umefanya jinai dhidi ya Waislamu wa Palestina na Kibla cha Kwanza cha Waislamu kiasi kwamba hata watu wasio Waislamu wanaendelea kulaani jinai hizo.