UN: Maelfu ya wakazi wa Gaza wamekimbia makazi na nyumba zao
-
Ukanda wa Gaza
Umoja wa Mataifa umetangaza kuwa, makumi ya maelfu ya wakazi wa eneo la Ukanda wa Gaza wamelazimika kukimbia nyumba zao kutokana na mashambulizi yanayoendelea kufanywa na utawala wa kizayuni wa Israel katika eneo hilo.
Ripoti iliyotolewa na Umoja wa Mataifa imesema kuwa, zaidi ya wakazi 38 elfu wa Ukanda wa Gaza wamelazimika kuwa wakimbizi kwa sababu ya mashambulizi ya mabomu na ndege za kivita za jeshi la Israel.
Ripoti hiyo imesema kuwa, idadi hiyo ya wakimbizi inajumuisha watu elfu 25 ambao nyumba na makazi yao yameharibiwa kwa mashambulizi ya mabomu na ndege za kivita za utawala wa Kizayuni wa Israel.
Hadi sasa Wapalestina zaidi ya 220 wameuawa shahidi na wengine zaidi ya 5,600 wamejeruhiwa. 60 kati ya waliouliwa shahidi ni watoto wadogo.
Maandamano yanaendelea kufanyika katika kila kona ya dunia kulaani jinai zinazoendelea za utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Wapalestina katika Ukanda wa Ghaza.
Siku za Jumamosi na Jumapili maelfu ya watu walifanya maandamano katika miji mikubwa ya Ulaya wakidhihiirisha hasira zao kutokana na jinai za utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Wapalestina. Aidha mandamano makubwa pia yamefanyika katika miji mikubwa ya Marekani na Canada kulaani jinai hizo za Israel dhidi ya Wapalestina.
Siku za Alhamisi na Ijumaa pia maandamano makubwa yalishuhudiwa katika nchi za Afrika kama vile Afrika Kusini, Kenya, Nigeria, Tunisia na Algeria ambapo waandamanaji walibainisha hasira zao kutokana na jinai za utawala haramu wa Israel dhidi ya Wapalestina.