Kuondoka na kurejea balozi wa Saudi Arabia nchini Qatar mwezi Juni
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i71592-kuondoka_na_kurejea_balozi_wa_saudi_arabia_nchini_qatar_mwezi_juni
Mwezi Juni umedhihiri kuwa na nafasi maalumu katika uhusiano wa miaka ya hivi karibuni baina ya Saudi Arabia na Qatar. Mwezi Juni miaka minne iliyopita, Saudi Arabia ilikata uhusiano wake wote na Qatar na kuiwekea vikwazo vya pande zote nchi hiyo ndogo ya Kiarabu. sasa hivi na baada ya kupita miaka yote hiyo, Saudia imeamua kumrejesha Qatar balozi wake katika mwezi wa Juni.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Jun 24, 2021 02:11 UTC
  • Kuondoka na kurejea balozi wa Saudi Arabia nchini Qatar mwezi Juni

Mwezi Juni umedhihiri kuwa na nafasi maalumu katika uhusiano wa miaka ya hivi karibuni baina ya Saudi Arabia na Qatar. Mwezi Juni miaka minne iliyopita, Saudi Arabia ilikata uhusiano wake wote na Qatar na kuiwekea vikwazo vya pande zote nchi hiyo ndogo ya Kiarabu. sasa hivi na baada ya kupita miaka yote hiyo, Saudia imeamua kumrejesha Qatar balozi wake katika mwezi wa Juni.

Mgogoro baina ya Saudi Arabia na Qatar ulipamba moto mwezi Juni 2017. Mohamed bin Salman, mrithi wa kiti cha ufalme wa Saudia anayependa makubwa, alidhani kwamba itakuwa rahisi kwake kuziweka chini ya udhibiti wake nchi zote ndogo ndogo za Kiarabu kama Qatar na nchi nyuingine dhaifu licha ya ukubwa wa ardhi yake kama vile Yemen. Bin Salman alikuwa anaziangalia nchi ndogo na dhaifu za Kiarabu kwa jicho la dharau na kujifanya nchi yake ni kaka mkubwa ambaye inabidi atiiwe hasa katika masuala ya kimataifa na siasa za nje. Kwa kweli Bin Salman na viongozi wa Saudia wanaona nchi nyingine ndogo na dhaifu za Kiarabu ni kama sehemu ya ardhi yake ambazo zinaweza kuwa huru katika masuala yao ya ndani, lakini hazipaswi kuipinga Riyadh katika masuala yao ya nje na misimamo yao ya kimataifa. 

Nchi dhaifu na ndogo kama Bahrain, kwa muda mrefu imesalimu amri mbele ya mashinikizo ya Saudia na inatii kila kinachotoka Riyadh. Hata hivyo Qatar muda wote imekuwa ikisisitizia uhuru wake wa kujiamulia yenyewe mambo yake yote bila ya kuingiliwa na madola mengine. Msimamo huo tab'an hauwezi kabisa kukubaliwa na viongozi wapenda jaha wa Saudi Arabia na ndio maana mwezi Juni 2017, Jumatatu asubuhi, ghafla moja mfalme Salman bin Abdulaziz wa Saudi Arabia alitangaza kukata uhusiano wake wote na Qatar. Siku hiyo hiyo nchi nyingine za Kiarabu za Bahrain, Umoja wa Falme za Kiarabu (Imarati) na Misri, nazo zikafuata mkumbo huo na kutangaza kukata uhusiano wao wote na Qatar.

Baada ya Qatar kufungiwa mipaka yote na kususiwa kikamilifu na nchi nne za Kiarabu, Iran ilijitokeza kumsaidia kikamilifu jirani yake huyo kwa kumfungulia zaidi mipaka yake yote na kumtumia bidhaa na mahitaji ya lazima

 

Si hayo tu, lakini pia nchi hizo zilifunga mipaka yao yote ya ardhini, angani na baharini, na kuwafukuza ghafla moja Waqatar wote na kila taasisi na shirika la Qatar katika nchi hizo. Waqatar walilalamikia vibaya udhalilishaji mkubwa waliofanyiwa wakati walipofukuzwa kwenye nchi hizo. Baada ya hapo nchi nne za Saudia, Imarati, Misri na Bahrain zilitoa masharti 13 magumu mno ya kuitaka Qatar iyatekeleze ndipo ziondoe vikwazo vyao. Hata hivyo Qatar ilisimama imara, na leo hii nchi hizo za Kiarabu, baada ya miaka mitatu na nusu, zimerejea zenyewe Qatar bila ya Doha kutekeleza sharti lao lolote.

Sasa hivi Saudi Arabia imeamua kurejesha balozi wake mjini Doha licha ya misimamo ya Qatar ya kuwa huru katika maamuzi yake kuwa imara zaidi kuliko huko nyuma. Jumatatu wiki hii, Mansour bin Khalid Aal Saud, balozi mpya wa Saudi Arabia, alikabidhi hati zake za utambulisho kwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Qatar mjini Doha. Hapa ni vyema tukaashiria mambo kadhaa kuhusu kubadilika siasa za Saudia mbele ya Qatar.

Kwanza ni kwamba kurejea balozi wa Saudi Arabia mjini Doha mwezi Juni 2021, mwezi ambao ndio huo huo alioondoka balozi wa zamani wa Saudia mjini humo yaani mwaka 2017, ni ushindi kwa serikali ya Qatar.

Nchi za Kiarabu zilizoizunguka nchi ndogo ya Qatar, yaani Saudia, Bahrain, Imarati na Misri ziliota ndoto ya kuilazimisha Qatar isalimu amri. Sasa zinakiri kufeli siasa zao

 

Jambo jengine ni kwamba, kurejea balozi wa Saudia mjini Doha, kuna maana ya kukiri Riyadh ubovu wa siasa zake za kutaka kuzidhibiti nchi ndogo na dhaifu za Kiarabu. Inaonesha wazi kwamba, viongozi wa Saudi Arabia wametambua kuwa, hakuna nchi yoyote inayoweza kuwa mkoa wa Saudia, bali kila nchi iko huru katika maamuzi yake ya ndani na nje.

Kufeli siasa za Saudi Arabia mbele ya Qatar kumetoa funzo kwa watawala wanagenzi na wasio na uzoefu wa Saudia hasa Mohamad bin Salman kwamba ulimwengu wa siasa haupaswi kuchukuliwa kwa mabavu na misimamo ya upande mmoja ya kutaka kila mtu atii amri zako. Kula mweleka Saudi Arabia mbele ya nchi ndogo ya Qatar kunazidi kuonesha kuwa, Saudi Arabia si dola lenye nguvu la kuweza kuzitishwa nchi nyingine siasa zake na mrithi wa kiti cha ufalme wa nchi hiyo ameonesha kivitendo jinsi alivyo mwanagenzi katika ulimwengu wa siasa na utawala.