Misri: Kuhitimishwa uingiliaji wa nchi ajinabi; sharti la kurejeshwa amani Syria
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i71798-misri_kuhitimishwa_uingiliaji_wa_nchi_ajinabi_sharti_la_kurejeshwa_amani_syria
Waziri wa Mambo ya Nje wa Misri amesema katika kikao cha mawaziri wa muungano wa kimataifa unaodai kupambana na Daesh kwamba, sharti la kurejesha amani huko Syria ni kukomesha uingiliaji wa nchi ajinabi nchini humo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jun 29, 2021 06:38 UTC
  • Misri: Kuhitimishwa uingiliaji wa nchi ajinabi; sharti la kurejeshwa amani Syria

Waziri wa Mambo ya Nje wa Misri amesema katika kikao cha mawaziri wa muungano wa kimataifa unaodai kupambana na Daesh kwamba, sharti la kurejesha amani huko Syria ni kukomesha uingiliaji wa nchi ajinabi nchini humo.

Sami Shoukry amesema kuwa ufumbuzi wa mgogoro wa wakimbizi wa Syria utaendelea kuwa kikwazo madhali hali ya mchafukoge na machafuko vingali vinaendelea kushuhudiwa na umoja kukosekana nchini humo. Waziri wa Mambo ya Nje wa Misri amebainisha hayo huko Rome katika kikao cha mawaziri wa muungano wa kimataifa wa muungano eti wa kupambana na kundi la kigaidi la Daesh. 

Kundi la kigaidi la Daesh 

Waziri wa Mambo ya Nje wa Misri amegusia mgogoro wa Syria katika vipengee mbalimbali na hatua ya makundi mbalimbali ya kigaidi ya kuyadhibiti baadhi ya maeneo ya nchi hiyo na kuweka wazi pia nafasi ya baadhi ya madola ya kieneo katika kuyakalia kwa mabavu maeneo ya ardhi ya Syria kwa madai ya kuzilinda nchi waitifaki ama kupambana na ugaidi. 

Mawaziri na wawakilishi wa nchi za Marekani, Italia, Canada, Misri, Ufaransa, Ujerumani, Ugiriki, Iraq, Ireland, Japan, Jordan, Lebanon, Uholanzi, Norway, Qatar, Saudi Arabia, Uturuki, Imarati, Uingereza na wawakilishi wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu (Arab League) na Umoja wa Ulaya wametoa taarifa mwishoni mwa kikao hicho na kutangaza uungaji mkono wao kwa matamshi ya Geir Pedersen Mjumbe Maalumu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Kuhusu Masuala ya Syria kwa ajili ya kutekeleza pande zote za azimio nambari 2254 la Baraza la Usalama la umoja huo; ikiwemo kuunga mkono daima usitishaji vita wa haraka katika ardhi yote ya Syria, kugawa misaada ya kibinadamu kwa amani na utulivu, na kupambana na ugaidi.