Bashar al Assad aapishwa rasmi kuwa Rais wa Syria
(last modified Sat, 17 Jul 2021 12:27:22 GMT )
Jul 17, 2021 12:27 UTC
  • Bashar al Assad aapishwa rasmi kuwa Rais wa Syria

Bashar al Assad leo amekula kiapo rasmi cha kuwa Rais wa nchi hiyo kwa kipindi kingine cha miaka miaka 7 mingine.

Televisheni ya al Mayadeen imeripoti habari hiyo na kusema kuwa, Bashar al Assad amekula kiapo bungeni mbele ya Spika wa Wabunge wa Syria.

Wakuu na shakhsia mbalimbali wa kisiasa, kichama, kidini, vyombo vya habari, watu wa elimu, utamaduni, michezo, sanaa, jamii na familia za mashahidi wameshiriki kwenye sherehe hizo.

Baada ya kuapishwa rasmi, Rais Bashar al Assad amehutubia bunge na kusema kuwa, mataifa ambayo yanaijua njia ya uhuru na ukombozi kamwe hayachoki katika kulinda na kupigania haki zao.

Wananchi wa Syria wakisherehekea ushindi wa Rais Bashar al Assad

 

Amesema, kuna baadhi ya watu walitaka kuigawanya vipande vipande Syria lakini wananchi wa nchi hiyo wametumia mshikamano wao kufelisha njama za maadui hao. 

Wananchi wa Syria walijitokeza kwa wingi sana katika uchaguzi wa hivi karibuni wa rais na huo ni ushahidi wa wazi jinsi mwamko wa kitaifa ulivyokita mizizi nchini Syria. Rais Bashar al Assad amesema, uzoefu uliopatikana kwenye uchaguzi huo umethibitisha kuwa, ni wananchi ndio wanaoupa uhalali utawala wa nchi.

Uchaguzi wa Rais ulifanyika mwezi uliopita nchini Syria na Rais Bashar al Assad alishinda kwa asilimia 95 katika uchaguzi huo.

Baada ya kutangazwa ushindi mutlaki wa Rais Bashar al Assad, wananchi wa miji tofauti ya Syria walimiminika mitaani na barabarani kufanya sherehe kwa siku kadhaa.