UNICEF yaonya kuhusu hali mbaya ya watoto milioni moja nchini Afghanistan
Mfuko wa Kuhudumia Watoto wa Umoja wa Mataifa (Unicef) umetahadharisha kuwa, watoto milioni moja wa Afghanistan wako katika hali mbaya na hatari ya kupoteza maisha kutokana na lishe duni.
Shirika hilo la Umoja wa Mataifa limeongeza kuwa, Afghanistan hivi sasa imekumbwa na mgogoro mkubwa sana wa kibinadamu huku mfumo wake wa afya na matibabu ukiwa unazidi kusambaratika.
Mwakilishi wa Unicef nchini Afghanistan, Salam al Janabi naye amesema kuwa, nchi hiyo hivi sasa imekumbwa na mgogoro mkubwa zaidi duniani wa kibinadamu. Amesema, mahitaji ya wananchi wa Afghanistan yanaongezeka siku baada ya siku huku mfumo wa afya na huduma za kijamii nchini humo ukizidi kusambaratika.

Vile vile amekumbusha kuwa, zaidi ya nusu ya wananchi wa Afghanistan wakiwemo watoto milioni 10 wanahitaji misaada ya haraka ya kibinadamu. Aslimia kubwa ya Waafghani yaani wananchi wa kawaida na viongozi wao wanasema kuwa, balaa lote hilo lililowakumba linatokana na siasa mbovu na zilizofeli za Marekani katika nchi yao.
Marekani na waitifaki wake walikuwa wameivamia na kuikalia kwa mabavu Afghanistan kwa zaidi ya miaka 20 lakini si tu siasa zao zimefeli na wamelazimika kukimbia nchini humo, bali pia siasa hizo za kibeberu zimeitumbukiza nchi hiyo ya Waislamu kwenye lindi kubwa la matatizo, njaa, ukosefu wa amani, ugaidi, vita, machafuko na kusambaratika mifumo ya matibabu, chakula, elimu na matatizo mengine mengi yasiyo na idadi.