Jeshi la Yemen lakomboa makumi ya maeneo waliyokimbia wavamizi
Vyombo vya habari vya Yemen vimetangaza kuwa, jeshi la nchi hiyo kwa kushirikiana na kamati za ukombozi za kujitolea za wananchi limefanikiwa kukomboa makumi ya maeneo ambayo madola vamizi yameyakimbia huko magharabi mwa nchi.
Televisheni ya al Mayadeen imenukuu duru za mstari wa mbele wa mapigano huko Yemen zikisema kuwa, baada ya muungano vamizi unaoongozwa na Saudia na Imarati kukimbia katika makumi ya maeneo ya mkoa wa al Hudaidah wa magharibi mwa Yemen, jeshi la nchi hiyo na kamati za kujitolea za wananchi jana Ijumaa liliingia kwenye maeneo hayo na kuyadhibiti.
Duru hizo zimeongeza kuwa, baada ya wanajeshi vamizi kuondoka kwenye maeneo hayo, vikosi vya serikali ya San'a vimeelekea upande wa uwanja wa ndege wa al Hudaidah ili kuukomboa. Jeshi la Yemen jana Ijumaa lilifanikiwa kudhibiti kiwanda cha kuzalisha chakula na maziwa cha al Hudaidah.
Duru za Yemen zimetangaza pia kuwa, askari wa muungano vamizi wa Saudi Arabia na Umoja wa Falme za Kiarabu (Imarati) wamechukua uamuzi wa ghafla wa kuondoka katika maeneo yao ya kusini na mashariki mwa mkoa wa al Hudaidah, magharibi mwa Yemen katika kile ambacho kinahesabiwa ni kujaribu kwenda kuwasaidia wapiganaji wa Abdu Rabuh Mansour Hadi mkoani Ma'rib. Uwezekano wa kuelekea Ma'rib wavamizi hao umepata nguvu baada ya askari hao wa muungano vamizi kuelekea upande wa mji wa al Makha (Mocha) wa magharibi mwa mkoa wa Taiz.
Vyombo vya habari vinasema kuwa, hesabu ya kinyumenyume ya kukombolewa kikamilifu mkoa wa Ma'rib imeanza baada ya wanajeshi wa serikali ya San'a kupata mafanikio makubwa katika medani za mapambano mkoani humo.