Ma'rib yashambuliwa vikali na wavamizi, al Houthi asema, wavamizi wamechanganyikiwa
Muhammad Ali al Houthi, Mkuu wa Kamati Kuu ya Mapinduzi ya Yemen amezungumzia hatua ya wavamizi wa nchi hiyo ya kukimbia kwenye maeneo mengi ya mkoa wa al Hudaidah na kushadidisha mashambulizi ya kipunguani nchini Yemen na kusema kuwa, wavamizi wanaongozwa na Saudia na Imarati wamechanganyikiwa.
Jana Ijumaa, vyombo vya habari vya Yemen vilitangaza kuwa, jeshi la nchi hiyo kwa kushirikiana na kamati za ukombozi za kujitolea za wananchi limefanikiwa kukomboa makumi ya maeneo ambayo madola vamizi yameyakimbia katika mkoa wa al Hudaidah wa magharabi mwa nchi.
Duru za Yemen zilitangaza pia hiyo jana kuwa, askari wa muungano vamizi wa Saudi Arabia na Umoja wa Falme za Kiarabu (Imarati) wamechukua uamuzi wa ghafla wa kuondoka katika maeneo yao ya kusini na mashariki mwa mkoa wa al Hudaidah, magharibi mwa Yemen katika kile ambacho kinahesabiwa ni kujaribu kwenda kuwasaidia wapiganaji wa Abdu Rabuh Mansour Hadi mkoani Ma'rib. Uwezekano wa kuelekea Ma'rib wavamizi hao umepata nguvu baada ya askari hao wa muungano vamizi kuelekea upande wa mji wa al Makha (Mocha) wa magharibi mwa mkoa wa Taiz.
Leo Jumamosi habari kutoka Yemen zinasema kuwa, ndege za muungano vamizi zimefanya mashambulizi makali mno dhidi ya mji wa Ma'rib, makao makuu ya mkoa wa Ma'rib ili kuzuia wanamapambano wa Yemen wasizidi kusonga mbele. Televisheni ya al Masira imetangaza kuwa, usiku wa kuamkia leo, muungano vamizi umefanya mashambulio 22 ya anga dhidi ya mji wa Ma'rib.
Televisheni hiyo imesema, lengo la mashambulizi hayo ni kuzuia kusonga mbele jeshi na vikosi vya kujitolea vya wananchi wa Yemen ambao wamekaribia kuukomboa mkoa huo muhimu sana ambao unahesabiwa kuwa ndiyo makao makuu ya serikali ya Abdurabuh Mansour Hadi, rais wa zamani wa Yemen aliyejiuzulu mwenyewe na kukimbilia Saudi Arabia.