Muungano wa Saudia unashirikiana na al-Qaeda vitani Yemen
Serikali ya Uwokozi wa Kitaifa Yemen inasema muungano vamizi wa Saudia ambao umekuwa vitani na nchi hiyo masikini unashirikiana na magaidi wakufurishaji wa kundi la Al Qaeda katika jinai dhidi ya watu wa Yemen.
Hayo yamesemwa na Abdul- Qadri al Murtadha, Mkuu wa Kamati ya Masuala ya Kisiasa katika Serikali ya Uwokozi wa Kisiasa ambaye ameongeza kuwa hivi karibuni wanamgambo wa muungano vamizi wa Saudia waliwanyonga wafungwa 10 wa kivita wa Jeshi la Yemen na Kamati za Kujitolea za Wananchi katika mji wa Al Hudaydah.
Al Murtadha amesema jinai hiyo imekuja siku moja tu baada ya kinara wa Al Qaeda nchini Yemen kukiri kuwa magaidi wa kundi hilo wanashirikiana na muungano vamizi wa Saudia katika medani kadhaa za kivita Yemen.
Ameongeza kuwa serikali ya Yemen imewasilisha malalamiko kuhusu jinai hiyo kwa Umoja wa Mataifa.

Juzi Khalid Saeed Batarfi, kinara wa Al Qaeda katika Bara Arabu (AQAP) alinukuliwa na Televisheni ya Al Mayadeen akisema magaidi wa kundi hilo wanapigana bega kwa bega na wanajeshi wa muungano vamizi wa Saudi Arabia wanaoshirikiana na wanamgambo watiifu kwa rais wa zamani wa Yemen Abd Rabbuh Mansur Hadi dhidi ya Jeshi la Kitaifa la Yemen na Harakati ya Ansarullah.
"Nafasi yetu katika kupigana dhidi ya Mahouthi (Ansarullah) iko wazi na hakuna anayeweza kukana hilo," amesema Batarfi. Mwezi Machi 2015, Saudi Arabia ilianzisha mashambulizi makubwa ya kivamizi dhidi ya wananchi wa Yemen kwa uungaji mkono kamili wa Marekani, utawala wa Kizayuni wa Israel, madola mengine ya kibeberu na kwa ushirikiano mkubwa na Umoja wa Falme za Kiarabu (Imarati) na baadhi ya nchi za Kiarabu kama Sudan pamoja na makundi kadhaa ya kigaidi kama vile Al Qaeda.