Waziri Mkuu wa zamani wa Israel, Benjamin Netanyahu aburuzwa mahakamani
Tovuti moja ya Kizayuni imeripoti kuwa, Benjamin Netanyahu, waziri mkuu wa zamani wa utawala wa Kizayuni wa Israel ameburuzwa mahakamani kwa tuhuma za ufisadi.
Toleo la mtandaoni la gazeti la Kizayuni la Jerusalem Post limeripoti habari hiyo na kuongeza kuwa, miongoni wa tuhuma zinazomkabili Benjamin Netanyahu ni rushwa, utapeli na udanganyifu. Netanyahu aliburuzwa mahakamani jana Jumanne.
Awali ilikuwa imepangwa kwamba, Nir Hefetz, msaidizi wa zamani wa Netanyahu afike mahakamani hapo kutoa ushahidi dhidi ya waziri mkuu huyo wa zamani wa Israel, lakini majaji wameakhirisha ushahidi wake hadi wiki ijayo.
Nir Hefetz ni mmoja wa mashahidi wakubwa wa kesi za ufisadi za Benjamin Netanyahu na alikuwa mtu wa karibu sana na Netanyahu kwa miaka mingi wakati Netanyahu alipokuwa waziri mkuu wa utawala wa Kizayuni.
Mwendesha mashtaka mkuu wa Israel amefungua mashtaka dhidi ya Netanyahu kwa kutumia vibaya madaraka yake ikiwa ni pamoja na hatua yake ya kujivutia uungaji mkono wa shirika la umeme kwa ajili ya kueneza siasa za kujinufaisha binafsi.
Jana Jumanne, mahakama ilifuatilia kesi ambayo ni maarufu kwa jina la "1000" na kesi ya zawadi zilizotolewa kinyume cha sheria maarufu kwa jina la "kesi ya 2000." Gazeti la Jerusalem Post limedai kuwa kesi hizo mbili zinaweza kuchukua miezi kadhaa au zaidi.
Netanyahu anakabiliana na kesi nyingi ikiwemo ile inayojulikana kwa jina la "kesi ya 4000" ambayo inahusu watu wake wa karibu akiwemo mkewe, waliotumia vibaya madaraka yake kupata nafasi ya kujitangaza katika vyombo vya habari.