Mateka wa Kipalestina aliyenyimwa matibabu afariki shahidi katika jela za Israel
Mateka wa Kipalestina aliyekuwa anashikiliwa katika jela ya utawala wa Kizayuni wa Israel amekufa shahidi baada ya kunyimwa matibabu.
Taarifa ya Alhamisi ya Idara ya Habari ya Palestina imemtaja Mpalestina huyo kuwa ni Sami Al Amour aliyekuwa na umri wa miaka 39.
Amour alitekwa nyara na utawala wa Kizayuni wa Israel mwaka 2008 na alikuwa na ugonjwa wa moyo na hali yake ya kiafya ilizorota akiwa kizuizini kutokana na kuwa hakupata matibabu.
Katika tukio jingine familia ya mateka Mpalestina, ambaye amesusia chakula kwa muda wa miezi minne kulalamikia hali mbaya katika jela za utawala haramu wa Israel, imesema hali yake ya kiafya imezorota vibaya sana.
Katika mahojiano na Al Alam, Televisheni ya Kiarabu ya Iran, Khaled Fasfous amesema hali ya ndugu yake, Kayed ni mbaya sana na yamkini akapoteza maisha wakati wowote ule. Amesema mfumo wa neva wa Kayed umeharibika kutokana na ususiaji chakula wa muda mrefu na sasa hawezi kuzungumza.
Kayed Fasfous, 34, kutoka mji wa Dura kusini mwa Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan amekuwa akisusia chakula kwa muda wa siku 125 sasa akitaka Israel iache kumshikilia bila kumfungulia mashitaka. Hivi sasa amelazwa katika hospitali ya Kizayuni ya Barzilai huko Ashkelon.
Hali kadhalika Wapalestina wengine wanne ambao wamesusia chakula katika magereza ya kuogofya ya Israel ni Alaa Aaraj, Hesham Abu Hawwash, Ayyad Hureimi, na Lo’ai al-Ashqar.
Zaidi ya Wapalestina 7,000 wanashikiliwa mateka katika jela za kugofya za utawala wa Kizayuni wa Israel huku wakiwa wananyimwa haki zao za kimsingi. Wapalestina hususia kula chakula mara kwa mara kulalamikia mateso na ukatili katika jela za Israel.