Jeshi la Yemen latoa onyo kali kwa askari wa Saudia
Msemaji wa jeshi la Yemen amewaonya vikali wanajeshi na mamluki wa muungano vamizi unaoongozwa na Saudi Arabia katika vita dhidi ya Yemen na kueleza kuwa, Riyadh na watifaki wake watabeba dhima ya matokeo mabaya ya chokochoko zao mpya.
Brigedia Jenerali Yahya Saree amesema hayo katika ujumbe aliotuma usiku wa kuamkia leo kwenye mtandao wa kijamii wa Twitter na kufafanua kuwa, muungano wa kijeshi wa Saudia umetekeleza mashambuilizi ya anga 65 dhidi ya Yemen ndani ya saa 24 zilizopita.
Ametahadharisha kuwa, vikosi vimamizi vijiweke tayari kupokea vipigo vikali kutoka kwa majeshi ya Yemen na vikosi vya kujitolea wananchi, kwa uchokozi huo mpya.
Mapema jana, jeshi la Saudia likishirikiana na mamluki wake, lilifanya operesheni ya hujuma za anga katika mikoa ya Yemen ya Sana’a, Dhamar, Sa’ada, na al-Jawf kwa madai ya kulipiza kisasi cha shambulio la makombora ya balestiki na ndege zisizo na rubani.
Hii ni katika hali ambayo, muungano huo vamizi unaoongozwa na Saudia huko Yemen hivi karibuni uliwanyonga mateka 10 wa kivita wa jeshi la Yemen. Wizara ya Mambo ya Nje ya Serikali ya Wokovu wa Kitaifa ya Yemen imesema kuwa hatua hiyo ni jinai ya kivita.
Utawala wa Saudi Arabia na mamluki wake wameenda mbali zaidi kwa kuwaua mateka wa vita wa Yemen, kuwakata vipandevipande na kutupa maiti zao baharini, unyama uliolaaniwa kote duniani.