Ripoti: Vibarua 50 wahamiaji walifariki dunia nchini Qatar mwaka 2020
Shirika la Kazi Duniani la Umoja wa Mataifa {ILO} limetangaza katika ripoti yake kuwa, wafanyakazi 50 wahamiaji walifariki dunia nchini Qatar mwaka jana 2020.
Ripoti hiyo ya Shirika la Kazi Duniani la Umoja wa Mataifa {ILO} imeeleza kuwa, zaidi ya wafanyakazi 500 walijeruhiwa vibaya, wakati taifa hilo la Ghuba likijiandaa kwa ajili ya fainali za mashindano ya soka ya Kombe la Dunia hapo mwakani 2022.
Ripoti hiyo imetolewa huku kukiwa na ukosoaji mkubwa kuhusu mazingira ya kazi kwa maelfu ya vibarua wahamiaji nchini Qatar.
Ripoti hiyo pia inawahusisha wale waliojenga viwanja kwa ajili ya Kombe la Dunia.

Ripoti hiyo ya Shirika la Kazi Duniani la Umoja wa Mataifa {ILO} imebainisha kuwa, sababu kuu ya vifo hivyo ni kuanguka huku ajali nyingi zikitokea mahali pa kazi.
Asasi na jumuiya mbalimbali za kutetea haki za binadamu zimekuwa zikikosoa kile kinachoelezwa kama, kukosekana mazingira salama kazini kwa vibarua wanaofanya kazi katika makampuni yanayojishughulisha na ujenzi wa viwanja vya soka nchini Qatar ambavyo vitatumika kwa ajili ya mashindano ya soka ya Kombe la Dunia hapo mwakani.
Hayo yanaripotiwa huku kukiendelea kushuhudiwa malalamiko kuhusiana na vitendo vya unyanyasi na mateso yanayofanywa dhidi ya vibarua na wafanyakazi katika mataifa mbalimbali ya Ghuba ya Uajemi ikiwemo Saudi Arabia.