Mchezaji wa tenisi kutoka Kuwait akataa kucheza na Muisraeli
Mchezaji maarufu wa mchezo wa tenisi kutoka Kuwait amepongezwa kwa hatua yake ya kujiondoa katika shindano moja la kimataifa baada ya kubainika kuwa alitakiwa ashindane na raia wa utawala haramu wa Israel.
Muhammad Al Awadi alijiondoa katika Mashindano ya J4 Dubai ambayo yamefanyika katika Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) kuanzia Januari 17 hadi 22.
Wanaharakati katika mitandao ya kijamii wamempongeza Mkuwaiti huyo kwa kukataa kuwa sehemu ya sera za kuanzisha uhusiano na utawala wa Kizayuni wa Israel ambao unazikoloni na kuzikalia kwa mabavu ardhi za Palestina.
Mwandishi maarufu wa Kuwait Saadie Mufreh Al Awadi amempongza mchezji tenisi huyo kutokana na msimamo wake imara na kusema hatua yake hiyo ni fahari kwa nchi yake.
Mwanaharakati Mpalestina Al Yasser Al Zaatrah ameandika katika ukurasa wake wa Twitter kuwa: "Nabusu paji la uso wako, umetoa pigo kwa wavamizi."
Naye mwandishi habari wa Misri Wael Kandil amesema kijana huyo Mkuwaiti mwenye umri wa miaka 14 ameamua kutocheza katika shindano hilo la kimataifa ili kutotia dosari historia katika maisha yake kwa kucheza na Mzayuni.
Naye mbunge mwandamizi wa Kuwait Osama al Shaheen ametuma ujumbe katika Twitter na kuandika: "Salamu na sukrani kwa shujaa wa Kuwait Muhammad al Awadi kutokana na hatua yake ya kupinga uhusiano wa kawaida wa kimichezo na Wazayuni."
Yusuf al Sanad, mwanachama wa Jumuiya ya Wasomi wa Ghuba ya Uajemi amesema kijana huyo shujaa wa Kuwait ametangaza kujitoa katika shindano hilo kama njia ya kubainisha kufungamana kwake na Wapalestina na kupinga ugaidi wa Israel.