Mzingiro wa Saudia huenda ukaua maelfu ya watoto wenye saratani Yemen
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i80052-mzingiro_wa_saudia_huenda_ukaua_maelfu_ya_watoto_wenye_saratani_yemen
Serikali ya Uokovu wa Kitaifa ya Yemen imesema maelfu ya watoto wa nchi hiyo wanaogua saratani wapo katika hatari ya kupoteza maisha kutokana na taathira hasi za mzingiro wa Saudi Arabia uliowekwa tangu mwaka 2015.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Feb 06, 2022 08:59 UTC
  • Mzingiro wa Saudia huenda ukaua maelfu ya watoto wenye saratani Yemen

Serikali ya Uokovu wa Kitaifa ya Yemen imesema maelfu ya watoto wa nchi hiyo wanaogua saratani wapo katika hatari ya kupoteza maisha kutokana na taathira hasi za mzingiro wa Saudi Arabia uliowekwa tangu mwaka 2015.

Waziri wa Afya ya Yemen, Taha al-Mutawakil amesema watoto 3,000 wa nchi hiyo maskini ya Kiarabu wanaosumbuliwa na maradhi ya kansa huenda wakapoteza maisha kwa kukosa huduma za afya kutokana na mzingiro huo wa Saudia.

Waziri huyo amebainisha kuwa, uvamizi na mzingiro wa Saudia dhidi ya Yemen umepelekea kufungwa Uwanja wa Ndege wa Sana'a, na hivyo nchi hiyo inashindwa kupokea dawa za nyuklia zinazohitajika kwa ajili ya kuwatibu wagonjwa wa kansa.

Waziri wa Afya ya Yemen amesisitizia udharura wa kufunguliwa uwanja huo wa ndege, ili kuruhusu kupelekewa nchini humo dawa na suhula nyingine za matibabu.

Watoto wenye saratani Yemen

Ameongeza kuwa, idadi ya wagonjwa wa saratani nchini Yemen imeongezeka maradufu kutokana na hatua ya muungano vamizi wa kijeshi unaoogozwa na Riyadh kuingiza nchini humo silaha haramu za kemikali.

Waziri wa Afya wa Yemen amesema hayo kwa mnasaba wa Siku ya Saratani Duniani na kueleza kuwa, siku hii inaadhimishwa wakati ambapo taifa hilo maskini la Kiarabu linasumbuliwa na mgogoro mkubwa wa kiafya, hususan ongezeko la wagonjwa wa kansa kutokana na mzingiro wa Saudia, na vilevile hatua ya muungano huo vamizi kuingiza nchini humo silaha haramu za kemikali.