UNICEF: Mamilioni ya watoto wa Yemen katika hatari ya kufa njaa
Mfuko wa Watoto wa Umoja wa Mataifa (UNICEF) umetangaza kuwa, mamilioni ya watoto wa Yemen wapo katika hatari ya kupoteza maisha kutokana na kusakamwa na njaa, huku muungano wa kivita unaoongozwa na Saudi Arabia ukiendelea kufanya mashambulizi na kuliwekea mzingiro wa kila upande taifa hilo maskini la Kiarabu.
Katika ujumbe uliotumwa kwenye mtandao wa kijamii wa Twitter jana Ijumaa, UNICEF imesema: Watoto wa Yemen wapo katika ncha ya kuaga dunia kwa njaa kali, si kutokana na uhaba wa chakula, bali kutokana na familia zao kushindwa kununua chakula chenyewe masokoni.
Shirika hilo la kushughulikia maslahi ya watoto la UN limeeleza kuwa, mamilioni ya watoto wa Yemen wanakabiliwa na njaa kutokana na kupungua kwa misaada ya kimataifa ya chakula.
Ripoti rasmi zinaonesha kuwa, watoto 300 wa Yemen wanafariki dunia ndani ya kila saa 24 kutokana na utapiamlo wa kiwango cha juu.
Katika hatua nyingine, takwimu za Wizara ya Afya ya Yemen zinaonesha kuwa, maelfu ya watoto wa nchi hiyo maskini ya Kiarabu wanaosumbuliwa na maradhi ya saratani huenda wakapoteza maisha kwa kukosa huduma za afya kutokana na mzingiro huo wa Saudia.
Umoja wa Mataifa umeonya kuwa, ikiwa vita havitomalizwa katika taifa hilo, basi Yemen itaelekea kwenye hali ambayo haitoweza kubadilishwa na kuingia kwenye hatari ya kupoteza kizazi kizima cha watoto nchini humo.