Bashar al-Assad: Magharibi imegeuza dunia kuwa msitu
-
Rais Bashar al-Assad wa Syria
Rais Bashar al-Assad wa Syria amekosoa sera za nchi za Magharibi dhidi ya nchi yake na kusema: "Magharibi imeigeuza dunia kuwa msitu."
Katika hotuba yake kwa mnasaba wa Siku ya Kimataifa ya Walimu, Bashar al-Assad amezungumza na walimu, wakufunzi na wafanyakazi wa sekta ya elimu nchini Syria, na kusema: "Sera inayofuatwa na nchi za Magharibi ni sera ya kutumia mabavu na kuigeuza dunia kuwa mithili ya msitu."
Ameongoza kuwa: Nchi za Magharibi zimethibitisha kuwa hazijali sheria za kimataifa na zinakanyaga taasisi za sheria za kimataifa na kuifanya dunia kuwa msitu."
Akieleza kuwa nchi za Magharibi zimetia fora katika kusema uongo na kuwahadaa walimwengu, Rais wa Syria amesema: Vita vya Ukraine vimewafedhehesha Wamaghabi mbele ya waungaji mkono wao.
Amesema Magharibi imetaifisha pesa za Russia, Syria na Libya, na kuhoji uko wapi uhuru wa kumili? Amesema madai yote ya Wamagharibi ni ya uongo na hawajali lolote isipokuwa kupora na kuidhibiti dunia.
Rais wa Syria hapo awali aliunga mkono operesheni maalumu ya kijeshi ya Russia nchini Ukraine katika mazungumzo yake ya simu na mwenzake wa Russia, Vladimir Putin.
Bashar al-Assad alilaani vitendo vya kichochezi vya Marekani na nchi za Magharibi dhidi ya Russia, akisema kuwa vitendo hivyo vitasababisha ghasia na machafuko.
Tarehe 24 Februari Russia ilianzisha operesheni maalumu ya kijeshi nchini Ukraine. Rais wa Russia, Vladimir Putin amesema hatua hiyo "inalenga kuwalinda watu ambao wamekuwa wakikabiliwa na uonevu na mauaji ya halaiki yanayofanywa na serikali ya Kyiv kwa miaka minane."

Rais Putin aidha ameeleza kuwa, lengo la Russia ni kuipokonya silaha Ukraine na kwamba haina lengo la kuikalia kwa mabavu nchi hiyo. Katika matamshi yake mengine, Rais Vladimir Putin wa Russia amezikosoa nchi za Magharibi kwa kupuuza wasiwasi wa Russia kuhusu usalama wa nchi hiyo na kwa kutuma huko Ukraine silaha mbalimbali za kisasa.
Russia imesisitiza mara kadhaa kwamba haitaruhusu nchi yake ikabiliwe na vitisho kupitia ardhi ya Ukraine.