Serikali ya Yemen: Bado tungali tunasubiri majibu kutoka kwa Saudia
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i81916-serikali_ya_yemen_bado_tungali_tunasubiri_majibu_kutoka_kwa_saudia
Naibu Waziri wa Habari wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa ya Yemen amesema kuwa, nchi yake bado inasubiri majibu kutoka kwa Saudi Arabia kuhusu hatua ya Sana;a ya kujitolea kusimamisha vita.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Mar 29, 2022 06:35 UTC
  • Serikali ya Yemen: Bado tungali tunasubiri majibu kutoka kwa Saudia

Naibu Waziri wa Habari wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa ya Yemen amesema kuwa, nchi yake bado inasubiri majibu kutoka kwa Saudi Arabia kuhusu hatua ya Sana;a ya kujitolea kusimamisha vita.

Fahmi al Yusufi amesema hayo leo Jumanne wakati alipohojiwa na mwandishi wa habari wa shirika la habari la IRIB na kuongeza kuwa, muungano vamizi unaoongozwa na Saudi Arabia sasa umeelewa kuwa kauwezi kuendelea na vita vya silaha nchini Yemen na njia pekee ya kutatua mgogoro huo ni kukomesha mashambulizi na jinai zake.

Vile vile amesema, ilichotarajia Sana'a ni kuona Saudia ikiipa umuhimu mkubwa hatua ya kujitolea Serikali ya Wokovu wa Kiataifa ya Yemen ya kusimamisha vita kwa upande mmoja, hata hivyo inavyoonekana ni kuwa, utawala wa kiimla wa Saudi Arabia na wavamizi wenzake, hawana uwezo wa kuchukua maamuzi, kwa sababu maamuzi yao yanatoka Washington na London.

Mahdi al Mashat, Mkuu wa Baraza Kuu la Kisiasa la Yemen

 

Wiki hii, Mahdi al Mashat, Mkuu wa Baraza Kuu la Kisiasa la Yemen la mjini Sana'a alitangaza pendekezo la kusimamisha vita na kusema kuwa wametoa muhula wa mwisho kwa muungano vamizi wa Saudia na Imarati kufikiria upya na kwa uzito wa hali ya juu suala la amani nchini Yemen na kukomesha hatua zozote zinazokwamisha kufikiwa makubaliano..

Alisema, kwa upande wake, jeshi la Yemen na vikosi vya kujihami vya wananchi wa nchi hiyo vimejitolea kusimamisha mashambulio ya makombora na ndege zisizo na rubani pamoja na operesheni zote za kijeshi dhidi ya Saudia kutokea angani, baharini na ardhi kwa muda wa siku tatu.