Wasaudia waua raia wasiopungua 3 Yemen, hawakuheshimu hata Ramadhani
Raia watatu wa Yemen wameuawa baada ya vikosi vya mpakani vya Saudi Arabia kushambulia kwa makombora na mizinga eneo la makazi ya raia katika mkoa wa Kaskazini Magharibi wa Sa'ada nchini Yemen, saa chache baada ya muungano vamizi unaoongozwa na Saudi Arabia, ambao umekuwa ukiendesha vita vya zaidi ya miaka 7 dhidi ya taifa la Yemen kukubali mapatano ya kusimamisha vita kwa miezi miwili.
Televisheni ya al-Masirah imeripoti kuwa, wahanga hao wameuawa wakati wanajeshi wa Saudia waliposhambulia wilaya ya Shada'a.
Zaidi ya hayo ni kwamba, wanajeshi wa muungano vamizi unaoongozwa na Saudi Arabia na mamluki wao wamekiuka mapatano ya kusitisha vita kwa kushambulia eneo la pwani ya Magharibi la Hudaydah mara 81 katika muda wa saa 24 zilizopita.
Mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa nchini Yemen, Hans Grundberg alitangaza usitishaji wa mapigano siku ya Ijumaa, akisema mapatano hayo ya miezi miwili yangeanza kutekelezwa jana Jumamosi.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres alisema mapatano hayo "yanapaswa kuwa hatua ya kwanza ya kumaliza vita vya Yemen," na kuzitaka pande husika kutumia fursa hiyo kwa ajili ya kuanzisha mchakato jumuishi wa kisiasa nchini Yemen."
Saudi Arabia na washirika wamekubali pendekezo la Umoja wa Mataifa la kusitisha vita huko Yemen siku chache baada ya operesheni ya aina yake ya jeshi na wapiganaji wa harakati ya wananchi wa Yemen ya Ansarullah dhidi ya taasisi za kistratijia ndani ya ardhi ya Saudi Arabia.