Kuwahamisha Wapalestina kwa nguvu ni jinai dhidi ya binadamu
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i83454-kuwahamisha_wapalestina_kwa_nguvu_ni_jinai_dhidi_ya_binadamu
Afisa mwandamizi wa Palestina amesema hatua ya utawala wa Kizayuni wa Israel wa kuwahamisha kwa nguvu Wapalestina sambamba na kubomoa vijiji katika eneo linalokaliwa kwa mambavu na utawala huo la Ukingo wa Magharibi ni jinai dhidi ya binadamu.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
May 10, 2022 03:33 UTC
  • Kuwahamisha Wapalestina kwa nguvu ni jinai dhidi ya binadamu

Afisa mwandamizi wa Palestina amesema hatua ya utawala wa Kizayuni wa Israel wa kuwahamisha kwa nguvu Wapalestina sambamba na kubomoa vijiji katika eneo linalokaliwa kwa mambavu na utawala huo la Ukingo wa Magharibi ni jinai dhidi ya binadamu.

Waziri wa Uadilifu wa Palestina Shalaldeh aliyasema hayo Jumatatu katika mkutano na waandishi habari akiwa ameandamana na mwendesha mashtaka mkuu wa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC), Karim Khan. Katika kikao hicho, Shalaldeh ametoa wito kwa ICC yenye makao yake The Hague ichunguze jinai hizo za Israel.

Ameongeza kuwa, jamii ya kimataifa, hasa ICC, inapaswa kuchukua hatua za kuwawajibisha wale wote waliotenda jinai za kivita na jinai dhidi ya binadamu huko Palesitna kuanzia waziri mkuu wa Israel hadi mlowezi na askari wa Kizayuni.

Aidha amesema kwa mujibu wa sheria za kimataifa, Wapalestina wana haki ya kupambana kutetea haki zao na kupigania uhuru wao.

Wakati ulimwengu ukiendelea kulaani hatua zisizo za kibinadamu za Israel huko Palestina, Naftali Bennett, Waziri Mkuu wa utawala huo ghasibu ametangaza kijeuri kabisa kwamba, utawala huo haujali chochote na kwamba, utachukua maamuzi yote yanayohusiana na msikiti wa al-Aqswa pamoja na mji wa Quds (Jerusalem) kwa madai kuwa ndio wenye mamlaka kwenye maeneo hayo.

Hayo yanajiri katika hali ambayo, utawala wa Kizayuni umepanga kupitisha mpango wa kujenga nyumba mpya zipatazo elfu nne katika eneo la Ukingo wa Magharibi, Palestina inayokaliwa kwa mabavu, tangazo ambalo limeendelea kulalamikiwa kieneo na kimataifa.