Iraq: Baada ya uchunguzi kukamilika tutatoa jibu kwa mashambulio ya Uturuki
Wizara ya mambo ya nje ya Iraq imelaani shambulio la kijeshi la Uturuki katika eneo la Sinjar na kusisitiza kuwa baada ya kukamilisha uchunguzi, itachukua hatua zinazolazimu dhidi ya Ankara.
Watu sita wameuawa katika shambulio la ndege isiyo na rubani ya Uturuki lililolenga majengo kadhaa katika mtaa wa Sanuni ulioko kwenye mji wa Sinjar mkoani Nainawa nchini Iraq. Baadhi ya duru za habari zimesema, watu wanne wameuawa katika hujuma hiyo.
Wizara ya mambo ya nje ya Iraq imeeleza katika taarifa kwamba, hatua hiyo ya Uturuki ni ukiukaji wa wazi wa mamlaka ya kujitawala ya nchi hiyo na kitisho cha wazi dhidi ya usalama wa raia ambao kadhaa miongoni mwao wameuawa kutokana na shambulio hilo.

Taarifa ya wizara ya mambo ya nje ya Iraq imeeleza pia kwamba itachukua hatua zinazotakiwa baada ya kukamilisha uchunguzi kuhusiana na shambulio la Uturuki; na ikaongezea kwa kusema, shambulio hilo ni hatua inayolenga moja kwa moja usalama wa Iraq na uthabiti wa watu wake na inahitaji msimamo wa pamoja wa kukabiliana nayo; msimamo ambao ni kusimama imara dhidi ya hatua yoyote ambayo lengo lake ni kueneza fujo na machafuko ndani ya Iraq.
Tangu mwezi Aprili mwaka huu Uturuki imeanzisha operesheni mpya za mashambulio ya kijeshi ya nchi kavu na angani kaskazini mwa Iraq kwa kutumia vikosi vyake maalumu pamoja na ndege zisizo na rubani kwa kisingizio cha kupambana na chama cha wafanyakazi wa Kurudistan ya Uturuki PKK.
Operesheni hiyo iliyopewa jina la "kufuli la koleo" inafuatia operesheni nyingine mbili zilizofanywa na jeshi la Uturuki mwaka 2020 huko kaskazini mwa Iraq kwa majina ya "kucha la chui" na "kucha la tai".../