Kuanza mgomo wa kula chakula wa wafungwa wa Kipalestina
Jumatatu ya juzi tarehe 22 Agosti, mateka wa Kipalestina wanaoshikiliwa katika jela za kuogofya za utawala wa Kizayuni wa Israel walianzisha mgomo usio na kikomo wa kula chakula wakilalamikia hatua za kidhalimu na maafisa wa utawala huo katika magereza.
Shirika la habari la Palestin al-Yaum limeinukuu Bodi ya Wafungwa Wapalestina ikisema kuwa, hali ya taharuki imetanda katika jela na magereza ya utawala wa Kizayuni, baada ya mateka hao wa Kipalestina kuanza mgomo wa kula chakula siku ya Jumatatu.
Kamati Kuu ya Dharura ya Wafungwa wa Kipalestina imetangaza kuwa, mgomo huo wa kula ulianza Jumatatu na kundi jingine la wafungwa litaanza leo Jumatano, kabla ya kuzinduliwa katika magereza na jela zote za Wazayuni wanakoshikiliwa kidhulma Wapalestina.
Mgomo huo wa kula ni muendelezo wa hatua za wafungwa wa Kipalestina, ambao wanalalamikia hali mbaya ya kibinadamu katika jela hizo za Wazayuni. Mateka zaidi ya 500 wa Kipalestina wamekataa kwenda kusikiliza kesi dhidi yao katika mahakama za kijeshi za Israel, tokea mwanzoni mwa mwaka huu hadi sasa.
Ripoti zinaonyesha kuwa, kuna wafungwa 4,600 wa Kipalestina katika magereza ya utawala wa Kizayuni wa Israel. Mateka hao wa Kipalestina wamekuwa wakikabiliwa na vitendo mbalimbali kama vya maudhi na mateso vinavyofanywa na maafisa magereza. Mwenendo wa vitendo hivyo siyo tu kwamba, unaendelea bali umechukua mkondo wa kuongezeka.
Ukweli wa mambo ni kuwa, kila mara kunapoongezeka mzozo, mvutano na mapigano baina ya Wazayuni na Wapalestina mateso dhidi ya Wapalestina katika magereza ya utawala huo ghasibu nayo huongezeka na kushadidi. Ni kama vile maafisa wa Israel humalizia hasira zao kwa wafungwa na mateka wa Kipalestina baada ya kushindwa kukabiliana na wanamapambano wa Palestina. Wafungwa wa Kipalestina daima wamekuwa wakihamishwa kutoka seli moja kwenda nyingine.
Baada ya kushadidi mateso na vitendo visivyo vya kibinadamu, wafungwa wa Kiplaestina waliamua kuanzisha mgomo wa kula chakula kuanzia siku ya Jumatatu kwa shabaha ya kulalamikia vitendo vya kidhalimu vya maafisa magereza katika jela za utawala huo ghasibu na vamizi. Lengo la mgomo huo wa kula ni kuzishinikiza mamlaka za magereza kutekeza makubaliano ili kwa njia hiyo mateka wa Kipalestina wapate haki zao hususan kuboreshewa mazingira ya magereza.
Mgomo wa kula chakula ni moja ya mbinu ambazo wafungwa wa Palestina hulazimika kuitumia ili kuzifikishia sauti yao fikra za waliowengi ulimwenguni na kufichua jinai za utawala haramu wa Israel. Mwaka 2019 zaidi ya mateka 400 wa Kipalestina waligoma kula chakula kwa muda wa siku tisa wakilalamikia kushikiliwa kwao kinyume cha sheria. Sheikh Khidhr Adnan mmoja wa wafungwa wa Kipalestina aliyeachiliwa huru na ambaye pia ni miongoni mwa viongozi wa Harakati ya Jihadul Islamu katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan amesema katika radiamali yake kuhusiana na mgomo wa kula chakula wa mateka wa Kipalestina kwamba: Kugoma kula chakula inahesabiwa kuwa njia ya heshima ya kuwafikishia walimwengu sauti ya kudhulumiwa taifa la Palestina ambalo linakaliwa kwa mabavu.
Nukta muhimu ni hii kwamba, utawala ghasibu wa Israel una kiwewe na hofu kubwa hata na mateka wa Kipalestina ambao kimsingi wako chini ya udhibiti wake katika magereza yake. Septemba mwaka jana (2021) Wapalestina watano wenye mfungamano na Harakati ya Jihadul Islami na mfungwa mmoja mwenye mfungamano na Harakati ya Fat’hi na ambao walihukumiwa vifungo vya muda mrefu gerezani, walifanikiwa kutoroka kutoka katika gereza na Gilboa, moja ya magereza yenye ulinzi mkali. Baadaye utawala huo ulifanikiwa kuwakamata tena mateka hao lakini ni baada ya fedheha kubwa iliyopata ya kutoroka mateka hao.
Jambo jingine muhimu ni kuwa, suala la wafungwa wa Kipalestina linaweza kuwa sababu ya umoja na mshikamano baina ya Wapalestina kwani takribani aghalabu ya Wapalestina ima wamepitia tajiriba na uzoefu wa kushikiliwa mateka au mmoja wa ndugu zao anashikiliwa mateka katika magereza ya utawala huo haramu.
Ni katika mkondo huo ndio maana siku yaJumatatu sambamba na kuanza mgomo wa kula chakula wa wafungwa wa Kipalestina katika magereza ya Israel, familia za wafungwa hao zilifanya mkusanyiko mbele ya Ofisi ya Shirika la Msalaba Mwekundu katika Ukanda wa Gaza. Dawood Shahab, mmoja wa viongozi waandamizi wa Harakati ya Jihadul Islamu ya Palestina aliliambia Shirika la Habari la Iran Press pambizoni mwa mkusanyiko huo kwamba: Taifa la Palestina na makundi yote ya Kipalestina yapo pamoja katika kuunga mkono vita vya wafungwa wa Kipalestina katika magereza ya Israel mpaka haki za Wapalestina hao zitakapotekelezwa.
Fares Sarafandi, mwanahabari wa Kanali ya Televisheni ya al-Alam huko Ramallah ametabiri kwamba, siku za usoni zitashuhudia mabadiliko muhimu katika faili la mateka wa Kipalestina. Hii ni kutokana na kuwa, suala la mateka wa Kipalestina likiingia hatua ya mgomo wa kula chakula, wakati huo kadhia haitakuwa ni ya wafungwa wa Kipalestina tu, bali suala hilo litakuwa ni la Wapalestina wote.
Kwa mujibu wa takwimu zilizotangazwa ni kuwa, takribani Wapalestina milioni 1 wametipia tajiriba ya kushikiliwa mateka katika magereza ya Israel kuanzia mwaka 1967 hadi sasa. Idadi hii inaundwa asilimia 20 ya taifa la Palestina. Kwa msingi huo, suala la mateka wa Kipalestina ni hasasi na nyeti mno la linaweza kusababisha kutokea mlipuko wa hali ya mambo katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na Ukanda wa Gaza.