Sep 15, 2022 02:29 UTC
  • Mahakama ya India yakataa ombi la Waislamu, ubaguzi unaendelea

Mahakama ya India imekataa ombi la Waislamu la kutupilia mbali shauuri la wanawake wa Kihindu la kutwaa msikiti wao katika mji wa Banaras.

Waislamu wa India huko Banaras, Uttar Pradesh, walikuwa wameiomba mahakama kutupilia mbali kesi iliyowasilishwa na wanawake wa Kihindu waliodai kumiliki msikiti wa Waislamu katika mji huo; hata hivyo mahakama imekataa ombi la Waislamu hao na kutangaza kwamba itasikiliza kesi hiyo. Mahakama hiyo pia imekubali kusikiliza ombi lililowasilishwa na wanawake wa Kihindu kwa ajili ya kupewa haki ya kuabudu katika Msikiti wa Gyanvapi.

Kamati ya usimamizi ya msikiti huo ilikuwa imemuomba jaji wa Wilaya ya Banaras huko Uttar Pradesh kutupilia mbali ombi la wanawake watano wa Kihindu kuabudu katika msikiti huo. Kamati hiyo iliiambia mahakama kuwa msikiti huo uliojengwa takriban miaka 600 iliyopita, ni mahali pa ibada kwa Waislamu.

Msimamo wa mahakama ya India wa kukataa ombi la Waislamu la kusimamisha kesi ya madai ya umiliki ya baadhi ya Wahindu kuhusu Msikiti wa Gyanvapi katika mji wa Banaras huko kaskazini mwa India, unaonyesha kuwa mfumo wa Mahakama na Serikali ya India unaendelea kufuata sera ya kukanyaga na kupuuza haki za Waislamu walio wachache katika nchi hiyo. 

Historia ya chama tawala cha Bharatiya Janata Party (BJP) nchini India katika kuvunjia heshima matukufu ya kidini ya Waislamu, ikiwa ni pamoja na kushambuliwa na kuharibu misikiti yao, ni moja ya nukta za giza za utendaji wa chama hicho katika miongo miwili iliyopita.

Kilele cha dharau na vitendo viovu vya Wahindu wenye msimamo mkali vya kuvunjiwa heshima matukufu ya Waislamu wa India kilishuhudiwa wakati wa utawala wa Narendra Modi (Waziri Mkuu wa sasa) katika jimbo la Gujarat mnamo 1992, wakati Waislamu zaidi ya 2000 walipouawa katika shambulio la Wahindu lililoharibu Msikiti wa Babri.

Kesi ya Msikiti wa Babri ilimalizwa yapata miaka mitatu iliyopita kwa uamuzi wa kibaguzi uliowapendelea Wahindu, na kwa msingi huo, ardhi ya Msikiti ulioharibiwa wa Babri walipewa Wahindu kujenga hekalu kwa uamuzi wa Mahakama Kuu ya India.

Maulana Arshad Madani, Katibu Mkuu wa Jamiat Ulamaa ya India anasema: "Hakuna mtu au taasisi yoyote inayoweza kukabidhi sehemu ambayo imekuwa msikiti kwa mamia ya miaka ili kuifanya hekalu; hivyo hapana shaka yoyote kwamba hukumu iliyotolewa na Mahakama ya Juu ya India kuhusiana na suala hili ni batili."

Katika miaka ya hivi karibuni, sera za ubaguzi za chama tawala nchini India dhidi ya Waislamu, zimewahamasisha Wahindu wenye misimamo mikali kuzidisha vitendo vya chuki na hujuma dhidi ya wafuasi wa dini hiyo ikiwemo kuharibu maeneo matakatifu na kuzidisha mateso na manyanyaso dhidi ya Waislamu katika miji mbalimbali. 

Mnamo mwaka wa 2020, takriban misikiti sita ilishambuliwa na kuharibiwa na Wahindu wenye itikadi kali, na maneno ya chuki ya maafisa wa serikali ya kitaifa ya India dhidi ya Waislamu yamekuwa na nafasi kubwa katika kuchochea jinai na uhalifu huo.

Wahindu wenye misimamo mikkali wakiharibu Msikiti wa Babri

Kuendelea kuharibiwa na kuchomwa moto misikiti, kuzuia sherehe na shughuli za kidini, kupiga marufuku utoaji vibali vya makazi kwa wahamiaji Waislamu, kufutwa kwa uhuru maalumu wa eneo la Kashmir na kimya cha jamii ya kimataifa mbele ya mashambulizi ya kikatili ya Wahindu wenye itikadi kali dhidi ya Waislamu ni miongoni mwa masuala yaliyochechea zaidi chuki dhidi ya Waislamu nchini India.

Kwa kulitilia maanani haya yote wachambuzi wa mambo wanasema kuwa, unyanyasaji wa Wahindu wenye itikadi kali dhidi ya Waislamu na maeneo yao matakatifu hautaisha hadi pale chama tawala cha Bharatiya Janata Party (BJP) nchini India kitakapoachana na sera ya kutumia mabavu na ubaguzi unaowalenga Waislamu.

Tags