Radiamali ya Syria kufuatia kuwepo vikosi ajinabi nchini humo
Damascus imekosoa kuwepo wanajeshi wa nchi za nje kaskazini mwa Syria.
Kwa mujibu wa shirika rasmi la habari la Syria (SANA) duru rasmi katika Wizara ya Mambo ya Nje ya nchi hiyo imesisitiza kuwa serikali ya Damascus inalaani kitendo cha kuwepo kinyume cha sheria vikosi maalumu vya Ufaransa na Ujerumani katika maeneo mawili ya Kobani na Manbij katika mkoa wa Aleppo kaskazini mwa Syria.
Serikali ya Damascus imesema kuwa kuwepo vikosi hivyo maalumu vya Ufaransa na Ujerumani katika maeneo hayo ni kinyume na sheria za kimataifa na kuitaja hatua hiyo kuwa isiyoweza kuhalalishika dhidi ya mamlaka na kujitawala nchi ya Syria.
Duru hiyo rasmi kutoka Wizara ya Mambo ya Nje ya Syria imeongeza kuwa kutolewa madai kuwa vikosi maalumu vya Ufaransa na Ujerumani vimetumwa huko Kobani na Aleppo eti kwa ajili ya kupambana na ugaidi hakuwezi kumpotosha mtu yoyote kwa sababu, mapambano dhidi ya ugaidi yanaweza kutekelezwa kwa kufuata sheria na kushirikiana tu na serikali halali ya Syria. Ripoti ya Wziara ya Mambo ya Nje ya Syria imeongeza kuwa wananchi wa Syria kwa mara nyingine tena wanasisitiza kuheshimiwa mamlaka na umoja wa ardhi yote ya Syria, kuipigania na kuilinda nchi yao hadi kuangamizwa kikamilifu magaidi wa kitakfiri nchini humo.
Baadhi ya duru za habari Jumanne wiki hii ziliarifu habari ya kutumwa kikosi cha wanajeshi wa Ujerumani kwa ajili ya kuvisaidia vikosi vya kidemokrasia vya Syria na kushiriki katika vita dhidi ya Daesh katika mji wa Manbij huko Syria; ambapo wanajeshi hao walitazamiwa kujiunga na washauri na wanajeshi wengine wa Marekani na Ufaransa wanaokaribia 500 ambao hivi karibuni waliwasili katika eneo hilo.