'Pango la Simba' kulipiza kisasi cha mauaji ya Wapalestina Jenin
Kundi la Muqawama wa Kiislamu la Arin al Usud (Pango la Simba) limesema litalipiza kisasi cha mauaji ya kikatili ya Wapalestina katika mji wa Jenin katika eneo la Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan.
Kundi hilo la mapambano lenye makao yake Nablus limesema katika taarifa kuwa, "Kama ambavyo daima huwa tunaahidi na kutekeleza ahadi yetu, hakuna shaka tutaliletea fakhari na izza taifa la Palestina. Leo hii pia tunaahidi kuwa, haitachukua muda kabla hatujalipiza kisasi kikali dhidi ya Wazayuni."
Limetoa mwito kwa Wapalestina kufanya maandamano katika ardhi zote zinazokaliwa kwa mabavu, kulaani jinai na umwagaji damu uliofanywa na wanajeshi Wazayuni katika mji wa Jenin.
Jana usiku Wapalestina wa Ukanda wa Gaza waliitikia mwito huo wa Arin al Usud na kufanya maandamano ya kutangaza uungaji mkono wao kwa makundi ya muqawama, sanjari na kulaani wimbi la ukatili wa Wazayuni maghasibu.
Baadhi ya waandamanaji hao wa Kipalestina walikusanyika nje ya makao makuu ya Shirika la Kimataifa la Msalaba Mwekundu mjini Gaza, na kutangaza kuwaunga mkono wafungwa wa Kipalestina mbali na kulaani mauaji ya Jenin.
Wakati huohuo, Brigedi ya Izzuddin Qassam, tawi la kijeshi la Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (HAMAS) imesisitiza pia kuwa, italipiza kisasi cha damu ya mashahidi wa Jenin.
Wanajeshi wa utawala wa Kizayuni wa Israel walishambulia mji wa Jenin katika eneo la Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan jana Jumanne na kuua shahidi Wapalestina wasiopungua 6 na kujeruhi makumi ya wengine.
Aidha Mohammad Shtayyeh, Waziri Mkuu wa Palestina ametoa mwito kwa mashirika ya kimataifa ya kutetea haki za binadamu kulaani jinai hizo za utawala wa Kizayuni wa Israel na mauaji yaliyofanywa jana na wanajeshi makatili wa Israel dhidi ya raia wa Palestina huko Jenin.