Marubani wa Israel wakataa kumpeleka Netanyahu Uingereza
Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni wa Israel amelazimika kuakhirisha safari yake ya kuitembelea Uingereza, baada ya marubani kadhaa wa utawala huo kukataa kumsafirisha kwa ndege katika nchi hiyo ya Ulaya mtawala huyo mwenye misimamo mikali.
Hayo yameripotiwa na gazeti la The Telegraph ambalo limefichua kuwa, serikali ya utawala wa Kizayuni imeshindwa kupata rubani ambaye yuko tayari kumpelekea Netanyahu nchini Uingereza. Netanyahu alipaswa kwenda Uingereza leo Alkhamisi.
Kwa mujibu wa Telegraph, huenda Netanyahu akalazimika kuakhirisha safari yake hiyo ya kuitembeleza Uingereza kwa jumla, kutokana na mzozo wa kisiasa ndani ya utawala huo. Utawala huo unashuhudia maandamano kwa miezi kadhaa sasa dhidi ya serikali yenye misimamo mikali ya Netanyahu.
Chanzo kimoja cha serikali ya Uingereza kimeliambia gazeti la Telegraph kuwa, "Tunafahamu kuwa marubani wa Kiisraeli wamekataa kumpeleka Netanyahu Uingereza.
Tukio kama hili lilishuhudiwa mwezi uliopita pia, baada ya marubani kukataa kumpeleka Waziri Mkuu huyo wa Israel nchini Italia. Maelfu ya Wazayuni walimiminika mitaani kushiriki maandamano makubwa zaidi dhidi ya Netanyahu yaliyopewa jina la "Kupambana na Udikteta." Waandamanaji walifunga barabara kuu zinazoelekea Uwanja wa Ndege wa Ben Gurion, kujaribu kumzuia Waziri Mkuu wa utawala huo asiende Italia.

Hata hivyo baada ya kufanikiwa kusafiri, mkalimani wa Kitaliano alikataa katakata kumfanyia kazi ya tarjumu Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni wa Israel, na kumtaja mwanasiasa huyo kama mtu hatari. Olga Dalia Padoa alisema amefikia uamuzi wa kutomfanyia kazi ya ukalimani Netanyahu, kwa kuwa si tu sikubaliani na misimamo yake ya kisiasa, lakini pia uongozi wake ambao ni hatari.
Maelfu ya walowezi wa Kizayuni wameandamana kwa wiki 11 mfululizo kupinga mpango wa mageuzi ya mahakama unaoshinikizwa na Netanyahu. Kutokana na mashinikizo hayo, yumkini Yoav Gallant, Waziri wa Vita wa Israel akatangaza hii leo kusimamishwa kwa mpango huo wa kuifanyika mageuzi idara ya mahakama ya utawala huo bandia.