Jun 21, 2016 14:58 UTC
  • Dunia yaendelea kuikosoa Bahrain kwa kumvua uraia Sh. Isa Qassim

Hatua ya utawala wa Bahrain kumvua uraia mwanazuoni mashuhuri wa Kiislamu Ayatullah Sheikh Isa Qassim, imeendelea kulaaniwa na asasi mbalimbali duniani, shakhsia mashuhuri na jamii ya kimataifa kwa ujumla.

Kamisheni Kuu ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa imelaani hatua hiyo na kusema kuwa imechukuliwa kwa jazba na kwamba inakiuka sheria za kimataifa.

Akiongea na waandishi wa habari mjini Geneva nchini Uswisi, Ravina Shamdasani, msemaji wa ofisi hiyo ya kushughulikia masuala ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa amesema haki ya uraia imedhaminiwa katika Hati ya Kimataifa ya Haki za Binadamu na mtu hawezi kupokonywa uraia pasina sababu za kimsingi.

Wakati huo huo, Ali Larijani, Spika wa Majilisi ya Ushauri ya Kiislamu yaani Bunge la Iran amekosoa uamuzi huo wa utawala wa Aal-Khalifa na kusema kuwa hatua hiyo ni dhihirisho tosha kwamba utawala huo upo katika ncha ya kusambaratika. Spika wa Bunge la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema hatua ya Manama kumpokonya uraia msomi mtajika wa Kiislamu itayatia madola yanayojidai kuwa watetezi wa haki za binadamu duniani katika mizani na mahakama ya umma.

Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran nayo imetoa taarifa kulaania hatua ya Bahrain ya kumvua uraia Ayatullah Isa Qassim. Taarifa hiyo imelaani vitendo vya utawala wa kifalme wa Bahrain kukandamiza viongozi wa kidini na kitaifa nchini humo sambamba na kuzuia uhuru wa kuabudu na kupora mali za waqfu za Wabahrain.

Jana Jumatatu, Utawala wa kiimla wa ukoo wa Aal-Khalifa wa Bahrain ulitangaza kumvua uraia mwanazuoni mkubwa na mashuhuri wa Kiislamu nchini humo Ayatullah Isa Qasim kwa madai kuwa ametumia vibaya nafasi yake kwa maslahi ya madola ya kigeni.

Tags