OIC yalaani kuuawa shahidi Wapalestina 3 Nablus
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i97724-oic_yalaani_kuuawa_shahidi_wapalestina_3_nablus
Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) imelaani kitendo cha wanajeshi makatili wa Israel cha kuwaua shahidi Wapalestina watatu katika mji wa Nablus, kaskazini mwa eneo la Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan linalokaliwa kwa mabavu na Wazayuni.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
May 22, 2023 23:49 UTC
  • OIC yalaani kuuawa shahidi Wapalestina 3 Nablus

Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) imelaani kitendo cha wanajeshi makatili wa Israel cha kuwaua shahidi Wapalestina watatu katika mji wa Nablus, kaskazini mwa eneo la Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan linalokaliwa kwa mabavu na Wazayuni.

Katika taarifa ya jana Jumatatu, Sekretarieti Kuu ya Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu imelaani mauaji hayo, na kuyataja kama jinai ya kihaini.

Kwa mujibu wa Wizara ya Afya ya Palestina, mbali na Wapalestina watatu kuuawa shahidi katika uvamizi wa askari wa Kizayuni, wengine saba wamejeruhiwa vibaya.

Vijana wa Kipalestina waliouawa shahidi mapema jana baada ya wanajeshi makatili wa utawala pandikizi wa Israel kuvamia kambi ya wakimbizi ya Balata huko Nablus ni Muhammad Abu Zaytoun, 32, Fathi Abu Rizk, 30, na Abdullah Abu Hamdan, 24.

Kabla ya hapo, Sekretarieti ya Jumuiya ya OIC ilitoa taarifa ikikemea kuendelea hujuma na uvamizi wa kila siku wa walowezi wa Kizayuni wakishirikiana na jeshi la Israel dhidi ya msikiti wa al-Aqsa.

Nembo ya OIC

Hii ni baada ya Itamar Ben-Gvir, Waziri wa Usalama wa Ndani wa utawala wa Kizayuni kuvamia katika Msikiti wa Al-Aqsa na kisha kuingia katika eneo la  Bab al-Maghreb. 

Mlolongo wa vitendo vya kiadui na uhasama vya wanajeshi wa Kizayuni dhidi ya raia wa Palestina katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu ungali unaendelea, na kila siku wanashambulia maeneo tofauti ya Palestina ili kufikia malengo yao ya kujitanua huku wakiwauwa shahidi, kuwajeruhi na kuwatia mbaroni raia wasio na hatia wa Palestina.