China yaitaka Israel iache chokochoko, uporaji wa ardhi za Wapalestina
China imeutaka utawala haramu wa Israel ukomeshe mara moja tabia yake ya uchokozi, kuchochea taharuki na kupora ardhi na rasilimali za Wapalestina hasa katika eneo la Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan.
Mwito huo umetolewa na Balozi wa China katika Umoja wa Mataifa, Geng Shuang na kusisitiza kuwa, taharuki imeshtadi eneo la Mashariki ya Kati tangu utawala wa Kizayuni uchukue hatua ya kusaini agizo la kubariki ujenzi zaidi ya vitongonji vya walowezi wa Kiyahudi kaskazini mwa Ukingo wa Magharibi, wiki iliyopita.
Kadhalika mwanadiplomasia huyo wa China amelaani kitendo cha hivi karibuni cha Itamar Ben-Gvir, Waziri wa Usalama wa Ndani wa utawala wa Kizayuni cha kuvamia Msikiti wa al-Aqsa na kisha kuingia katika eneo la Bab al-Maghreb.
Balozi wa China katika Umoja wa Mataifa ameeleza kuwa, hatua ya waziri huyo wa Kizayuni mwenye misimamo ya kufurutu ada haitakuwa na matokeo mengine ghairi ya kuvuruga zaidi hali ya mambo katika eneo la Asia Magharibi.
Waziri wa Usalama wa Ndani ya utawala wa Israel mbali na kufanya uafriti wa kuvamizi Masjidul Aqsa alidai kuwa, utawala huo pandikizi ndio utakaosimamia eneo la Bab al-Maghreb ndani ya msikiti huo mtakatifu wa Waislamu.
Hii ni katika hali ambayo, Msikiti wa Al-Aqsa unajulikana kuwa nembo kuu ya utambulisho muhimu wa Kiislamu na Palestina mjini Beitul Muqaddas, licha ya utawala wa Israel kujaribu kuharibu umuhimu huo. Aidha kusimama kidete na kuwa macho wananchi wa Palestina kumeufedhehesha utawala wa Kizayuni na kuufanya ushindwe kufikia malengo yake maovu dhidi ya Waarabu na Waislamu.