Jeshi la Israel laua na kujeruhi makumi ya Wapalestina Jenin
Jeshi la utawala wa Kizayuni Israel limeua na kujeruhi makumi ya Wapalestina katika mji wa Jenin, kaskazini mwa eneo la Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan linalokaliwa kwa mabavu na Wazayuni.
Kwa mujibu wa Wizara ya Afya ya Palestina, mbali na Wapalestina watatu kuuawa shahidi katika uvamizi wa askari wa Kizayuni huko Jenin, wengine 37 wamejeruhiwa vibaya.
Shirika la habari la WAFA limenukuu taarifa ya wizara hiyo ikisema kuwa, vijana wa Kipalestina waliouawa shahidi mapema leo baada ya wanajeshi makatili wa utawala pandikizi wa Israel kuwashambulia kwa risasi ni Khaled Asa’sah, 21, Ahmad Saqer, 15, na Qassam Abu Siryie, 29.
Habari zaidi zinasema kuwa, makabiliano makali yameshuhudiwa baina wanajeshi wa Israel na wanamuqawama wa Palestina katika kambi ya wakimbizi ya Jenin na karibu na eneo la al-Jabriyat, ambapo magari kadhaa yamechomwa moto.
Televisheni ya TV7 ya Kizayuni imeripoti kuwa, wanajeshi sita wa utawala huo pandikizi unaoua watoto wa Kipalestina kila leo, wamejeruhiwa kwenye makabiliano hayo mjini Jenin.
Mlolongo wa vitendo vya kiadui na uhasama vya wanajeshi wa Kizayuni dhidi ya raia wa Palestina katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu ungali unaendelea, na kila siku wanashambulia maeneo tofauti ya Palestina ili kufikia malengo yao ya kujitanua huku wakiwauwa shahidi, kuwajeruhi na kuwatia mbaroni raia wasio na hatia wa Palestina.
Wapalestina 160 wakiwemo watoto wadogo 28 wameuawa shahidi kwenye mashambulizi hayo ya kichokozi ya vikosi vamizi vya Israel tangu mwanzoni mwaka huu 2023 hadi sasa.