Sababu zilizotolewa na Taliban kuhusu kutoruhusu kusoma wasichana wa Afghanistan
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i99232-sababu_zilizotolewa_na_taliban_kuhusu_kutoruhusu_kusoma_wasichana_wa_afghanistan
Zabihullah Mujahid, msemaji wa kundi la Taliban la Afghanistan amesema kuwa, kuzuiwa wasichana nchini humo, kusoma masomo ya zaidi ya darasa la sita ni jambo la dharura kwa hivi sasa hadi pale vitabu vya masomo vitakapofanyiwa marekebisho.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jun 26, 2023 23:16 UTC
  • Sababu zilizotolewa na Taliban kuhusu kutoruhusu kusoma wasichana wa Afghanistan

Zabihullah Mujahid, msemaji wa kundi la Taliban la Afghanistan amesema kuwa, kuzuiwa wasichana nchini humo, kusoma masomo ya zaidi ya darasa la sita ni jambo la dharura kwa hivi sasa hadi pale vitabu vya masomo vitakapofanyiwa marekebisho.

Amesema, mtalaa wa hivi sasa wa masomo nchini Afghanistan umetoka kwa nchi za Magharibi na wamebebeshwa tu wananchi wa Afghanistan.

Ijapokuwa matamshi hayo ya Zabihullah Mujahid ya kuzuiwa wasichana wasiendelee na masomo baada ya kumaliza darasa la sita nchini Afghanistan yanahesabiwa ni msimamo rasmi wa kundi la Taliban, lakini uhalisia wa mambo unaonesha kuwa jamii ya Afghanistan haikubaliani na msimamo huo kama ambavyo jamii ya kimataifa nayo tangu zamani inapinga jambo hilo. Sababu zake ni kwamba, hivyo vitabu vya masomo vilikuwa vinafundishwa maskulini na serikali zilizopita na havionekani kuwa ni kama hivyo linavyodai kundi la Taliban. Jamii ya Afghanistan ni ya watu wanaoishi kijadi na si rahisi kusomeshwa mambo ambayo yanakinzana na dini na utamaduni wao. Ingekuwa hivyo, basi maulamaa na wananchi Waislamu wa Afghanistan wasingeruhusu hata siku moja kuendelea kusomeshwa mambo yanayokinzana na dini na utamaduni wao.

Molavi Moflih, mtaalamu wa masuala ya kisiasa anasema: Tab’an hisia kali za kundi la Taliban kuhusu vitabu vya masomo kwa watoto wa kike zinapaswa kuzingatiwa na tunatambua kuwa wanataka kulea kizazi salama cha watoto wa kike katika jamii ya Afghanistan, lakini swali muhimu linalojitokeza hapa ni kwamba, huo mfumo wa masomo wa Taliban unashindwaje kufanyia marekebisho vitabu hivyo wakati maalumu kama wakati wa likizo ya muda mrefu wa msimu wa joto kali ili kutowazuia wasichana kuendelea na masomo na wakati huo huo kuwakabidhi vitabu wanavyoona vinafaa kwa mfumo wao wa masomo?

Zabihullah Mujahid, msemaji wa kundi la Taliban la Afghanistan

 

Matamshi ya msemaji wa kundi la Taliban kwamba wao hawakusema wamepiga marufuku wasichana kusoma bali wamesimamisha kwa muda tu masomo yao hadi vifanyiwe marekebisho vitabu vyao wa kusomea, yanaonesha kuwa ni katika juhudi za kundi hilo za kupunguza mashinikizo ya kimataifa kwa Taliban. Mtazamo huo unapata nguvu hasa tunapoangalia azimio lililotolewa kwenye kikao cha hivi karibuni cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ambalo limesema wazi kuwa serikali ya Taliban huko Afghanistan haitoweza kutambuliwa kimataifa hadi pale kundi hilo litakapoheshimu haki za wanawake zikiwemo za kupata elimu.

Inaonekana wazi kwamba azimio hilo la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ni onyo kwa kundi la Taliban ambalo linapigania kufa na kupona kutambuliwa utawala wake nchini Afghanistan. Ijapokuwa huko nyuma kundi la Taliban lilisema kwamba limewazuia wasichana kusoma kutokana na misimamo yake ya kifiqhi, lakini dini tukufu ya Kiislamu si tu haiwazuii wasichana kusoma, bali inatilia mkazo sana watu wote wasome wakiwemo wasichana ili kwa njia hiyo jamii ya Waislamu iwe na watu bora kielimu na kimaadili kwa ajili ya kulea vizazi bora vya baadaye. Ni kwa sababu hiyo pia ndio maana maulamaa wa Kiislamu hawaungi mkono msimamo wa kundi la Taliban wa kuwazuia wasichana kupata elimu.

Asadullah Zaeri, mtaalamu mwingine wa masuala ya kisiasa nchini Afghanistan anasema: Katika zama zetu hizi ambazo ni zama za elimu, ustawi na maendeleo, si rahisi kuwazuia kusoma wasichana hata katika jamii kama ya Afghanistan ambayo inaishi kijadi. Sababu yake ni kuwa jamii hiyo inahitajia mno wanawake katika sekta zake mbalimbali zikiwemo za tiba na matibabu kama ambavyo wanawake waliosoma wanaweza kuwalea vizuri watoto na kuitunuku jamii ya Afghanistan kizazi cha wasomi wanaoweza kujiletea ustawi na maendeleo makubwa.

Alaakullihaal, msemaji wa kundi la Taliban amedai kwamba huko nyuma asilimia 30 tu ya maeneo ya Afghanistan yaliwezekana kutolewa elimu kwa wanafunzi lakini sasa shule zimeenea kwa asilimia mia moja katika maeneo, majimbo, miji na vijiji vyote vya Afghanistan. Hata tukikubaliana na madai hayo na tukikubali kwamba hiyo ni habari nzuri inayoonesha kuwa kundi la Taliban linaipa umuhimu elimu nchini Afghanistan, lakini inaonekana wazi kabisa kwamba, jamii ya Afghanistan haiwezi kukubaliana na suala la kuzuiwa wasichana kuendelea na masomo baada ya kumaliza darasa la sita. Jamii ya kimataifa pia haiwezi kukubaliana na jambo hilo hasa kwa kuzingatia kuwa ni muda mrefu sasa umepita, wasichana wa Afghanistan wamezuiwa kupata haki yao ya elimu.

Kwa kuzingatia yote hayo tutaona kuwa, kama kweli kundi la Taliban lilikuwa na nia ya kufanyia marekebisho vitabu vya masomo, lingekuwa limeshafanya hivyo tangu zamani na wasichana wa Kiafghani wangelikuwa wanaendelea na masomo yao bila ya kizuizi chochote.

Wasichana wa Afghanistan wanapenda kuwa na elimu kama walivyo na elimu wasichana wenzao katika kona mbalimbali za dunia. Si hayo tu, lakini pia inasemwa kuwa, wasichana wa viongozi wengi wa kundi la Taliban wanaendelea na masomo kwa uhuru na kwa juhudi kubwa katika nchi nyingine kama Qatar na Pakistan bila ya viongozi hao kudai kuwa mifumo ya masomo ya nchi hizo ni ya Magharibi.