Kuzidi kuporomoka nafasi ya Netanyahu huko Israel
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i99270-kuzidi_kuporomoka_nafasi_ya_netanyahu_huko_israel
Matokeo ya uchunguzi wa maoni ya hivi karibuni kabisa uliofanywa na vyombo vya habari vya utawala ghasibu wa Israel yanaonyesha kuwa, mapenzi na uungaji mkono kwa Benjamin Netanyahu unazidi kuporomoka huku vyama tanzu katika serikali yake vikizidi kumuacha mkono.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jun 27, 2023 22:51 UTC
  • Kuzidi kuporomoka nafasi ya Netanyahu huko Israel

Matokeo ya uchunguzi wa maoni ya hivi karibuni kabisa uliofanywa na vyombo vya habari vya utawala ghasibu wa Israel yanaonyesha kuwa, mapenzi na uungaji mkono kwa Benjamin Netanyahu unazidi kuporomoka huku vyama tanzu katika serikali yake vikizidi kumuacha mkono.

Tangu mwaka 2009 hadi sasa, Netanyahu hajawahi kushikilia wadhifa wa Waziri Mkuu wa Israel kwa zaidi ya mwaka mmoja. Netanyahu ambaye ni kiongozi wa chama cha Likud amewahi kushika wadhifa wa Waziri Mkuu wa Israel na kuunda serikali ima kupitia muungano na vyama vya mrengo wa kulia, au muungano na washindani wake na hivi karibuni kupitia muungano na Wazayuni wenye misimamo ya kufurut ada katika dini.

Mnamo mwaka 2012 baada ya miaka 12, Netanyahu alikabidhi wadhifa wa Waziri Mkuu kwa mshindani wake ambaye nukta pekee ya pamoja baina yao ni upinzani wake kwa Netanyahu kwani wawili hawa hawakuwa na ukaribu sana wa kifikra na kimrengo.

Pamoja na hayo, mzozo mkubwa na harakati za Netanyahu zilisababisha umoja na muungano wa washindani hawa usidumu isipokuwa kwa mwaka mmoja tu na kwa kusambaratika baraza la mawaziri, ikalazimu kuitishwa uchaguzi wa kabla ya wakati na kumrejesha tena madarakani Netanyahu.

Licha ya hayo, baada ya kupita miezi sita tu tangu Netanyahu aingie tena madarakani, matokeo ya uchunguzi wa maoni wa Kanali ya 12 ya utawala wa Kizayuni wa Israel yanaonyesha kuwa, kama uchaguzi utafanyika leo, basi vyama tanzu na vinavyounda serikali ya sasa ya Netanyahu vitafanikiwa kupata viti 54 tu kati ya 120 vya Bunge la Israel, yaani viti 10 pungufu ikilinganishwa na viti 64 vya sasa ambavyo viliufanya uunde serikali.

Benjamin Netanyahu, Waziri Mkuu wa utawala haramu wa Israel

 

Moja ya sababu muhimu za kuundwa kwa baraza hili la mawaziri ni uwepo wa watu wenye misimamo mikali na wabaguzi wa rangi. Kuwa na misimamo mikali na ubaguzi wa rangi baadhi ya wajumbe wa baraza la mawaziri hilo limeandaa uwanja na mazingira ya kushadidi machafuko ya kijamii na kisiasa pamoja na kutetereka mafungamano.

Aidha baraza la mawaziri la Netanyahu limechukua hatua za kudhoofisha mgawanyo wa madaraka wa serikali na mfumo wa mahakama wa utawala ghasibu wa Israel. Baraza hili la mawaziri liliidhinisha kile kinachojulikana kama mpango wa mageuzi ya mahakama kwa kuungwa mkono na bunge.

Katika mpango huu, mamlaka ya mfumo wa mahakama yatapunguzwa na nguvu na nafasi ya utendaji na bunge itaimarishwa katika utawala huu.

Viongozi wa upinzani na waandamanaji wanaamini kuwa, mageuzi yaliyofanywa na baraza la mawaziri la Netanyahu katika mfumo wa mahakama yanadhoofisha mfumo wa mahakama na ni jaribio la Netanyahu la kuzuia kesi zake tatu za ufisadi na kupokea hongo. Aidha wanaamini kuwa, hatua hizi za baraza la mawaziri zitaupelekea hatua kwa hatua utawala wa Kizayuni kuelekea upande wa migogoro na vita vya wenyewe kwa wenyewe.

 

Waandamanaji wanasema kuwa, mpango huo wa mageuzi ya mahakama utatoa pigo kubwa kwa demokrasia, kwani utapunguza ushawishi wa Mahakama ya Juu (chombo cha juu zaidi cha mahakama cha utawala wa Kizayuni) katika mchakato wa kuidhinisha sheria za msingi na kuruhusu Wabunge wa Bunge la Israel Knesset kuchelewesha kuidhinishwa kwake.

Kwa msingi huo, waandamanaji katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu (Israel) ambao mpaka sasa wamefanya maandamano kwa wiki 25 mtawalia, sambamba na kupinga mpango wa mageuzi ya mahakama, wanataka baraza la mawaziri la Netanyahu livunjwe.

Netanyahu alilazimika kuachana na mpango wa mageuzi ya mahakama kutokana na kuendelea kwa maandamano, lakini bado maandamano ya wananchi hayakukoma. Wiki 25 mfululizo za maandamano pia zinaonyesha ukubwa wa chuki za umma na fikra za waliowengi katika maeneo yanayokaliwa kwa mabavu dhidi ya Netanyahu na baraza lake la mawaziri lenye misimamo ya kufurutu ada.