Jinamizi la Wazayuni kufuatia kusambaratika ukiritimba wao katika nguvu ya anga
Gazeti la Kiebrania la Maariv limeripoti kuwa uchunguzi wa duru za kijeshi za utawala wa Kizayuni wa Israel unaonyesha kuwa uwezo wa anga hususan wa ndege zisizo na rubani za harakati ya Hizbullah ya Lebanon umeongezeka ili kukabiliana na nguvu za anga za utawala huo ghasibu.
Kwa mujibu wa ripoti ya gazeti hilo la lugha ya Kiebrania, duru za kijeshi za Kizayuni zimekiri kwamba, nguvu ya ulinzi wa anga ya Hizbullah ya Lebanon imeshuhudia mabadiliko makubwa katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, ambayo yanaweza kupunguza pakubwa pengo la uwezo wa harakati hiyo na nguvu ya anga ya utawala wa Kizayuni.
Ripoti hiyo inasema: Uamuzi wa Hizbullah ya Lebanon wa kuamilisha mifumo ya ulinzi wa anga ya SA8, SA22 kutoka Russia ni mabadiliko ya kimsingi ambayo yataiwezesha kuwa na uwezo wa kusitisha shughuli za Jeshi la Anga la Israel.
Mnamo mwaka 2019, Hizbullah ya Lebanon ilijaribu kulenga ndege isiyo na rubani ya Israel ya Hermes 450 kwa kombora la SAM-8 ili kukabiliana na shambulio la ndege hiyo ya kivita ya utawala wa Kizayuni katika vitongoji vya kusini mwa Beirut, na huo ukawa mwanzo wa tishio la Hizbullah la kutungua ndege za kivita za Israel zisizo na rubani.
Kabla ya hapo Meja Jenerali mmoja katika kikosi cha akiba katika jeshi la utawala haramu wa Israel sambamba na kuonyesha wasiwasi wake kuhusu nguvu za kijeshi za Hizbullah ya Lebanon alisisitiza kuwa, vikosi na makombora ya Hizbullah yana uwezo wa kufika katika sehemu yoyote ya ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu ambazo zimepachikwa jina bandia la Israel.
Amiram Levin, ambaye pia aliwahi kufanya kazi katika shirika la kijasusi Mossad, alisema: Hizbullah inaweza kulenga maeneo makubwa na yenye watu wengi kwa makumi ya maelfu ya makombora.
Vyombo vya habari vya utawala wa Kizayuni vimekiri kuwa makombora ya Hizbullah yenye uwezo wa kulenga shabaha kwa kiwango cha juu sasa yanawakosesha usingizi maafisa wa usalama na kijeshi wa utawala huo.
Hivi karibuni Hizbullah ya Lebanon ilifanikiwa kuiangusha ndege isiyo na rubani ya kijasusi ya utawala wa Kizayuni iliyokuwa imeingia katika ardhi ya Lebanon kutoka upande wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni vya "Zareit" kaskazini mwa Palestina inayokaliwa kwa mabavu.
Picha zilizochapishwa za operesheni hiyo zilionyesha kwamba adui wa Kizayuni alijaribu kurejesha udhibiti wa ndege hiyo isiyo na rubani au droni, lakini alishindwa kufanya hivyo. Droni hiyo ilikuwa ya aina ya R-Copter 1000 na ilikuwa na kamera mbili za ubora wa juu.
Kabla ya hapo na katika miaka ya hivi karibuni, Hizbullah imeuonya utawala wa Kizayuni kwamba haitanyamaza tena mbele ya ukiukwaji wa anga ya Lebanon unaofanywa na ndege zisizo na rubani za utawala huo.
Kufuatia mzozo wa maeneo ya gesi ya Lebanon ambayo utawala wa Kizayuni ulikusudia kuyachimba na hivyo kupora utajiri huo bila mapatano kuhusu eneo hilo linalozozaniwa, Hizbullah ilituma ndege tatu zisizo na rubani kwenye machimbo hayo ya gesi. Oparesheni ya droni hizo za Hizbulla ilikuwa yenye mafanikio makubwa kwani kikosi cha anga cha jeshi la utawala wa Kizayuni hakikufanikiwa kuzitambua, jambo ambalo kwa mara nyingine lilionyesha uwezo wa ndege zisizo na rubani za Hizbullah.
Utawala wa Kizayuni unataka kudhibiti uwezo wa Hizbullah ili kuendelea na shughuli zake za kijasusi nchini Lebanon, lakini kwa upande mwingine, unaogopa kuviziwa na Hizbullah.
Hizbullah ya Lebanon imeweza kuleta mlingano mpya katika vita vya anga vinavyozuia uwezo wa utawala wa Kizayuni kujipenyeza unavyotaka katika anga ya Lebanon, na viongozi wa usalama na kijeshi wa Israel wenyewe wamekiri ukweli huo.
Kwa mujibu wa wachunguzi na wachambuzi wa masuala ya kijeshi na kisiasa, Hizbullah ya Lebanon katika miaka ya hivi karibuni imefanikiwa kuibua mlingano mpya katika vita vya anga kwa lengo la kuuzuia utawala wa Kizayuni usiingie kwenye anga ya Lebanon, jambo ambalo linawatia wasiwasi Wazayuni.
Kinachoongeza wasiwasi wa utawala wa Kizayuni ni mafanikio ya makundi ya muqawama ya Palestina katika uwezo wa ndege zisizo na rubani na ulinzi wa anga.
Wahandisi wa Hizbullah wamefanikiwa kujiundia makombora yanayovurumishwa yakiwa yamebebwa begani aina ya Strela 2 na wameyafanyia majaribio kwa ufanisi.
Strela 2 ni kombora lenye uwezo wa kuvurumishwa hadi umbali wa mita zaidi ya 1500 kutoka nchi kavu kuelekea angani. Kombora hilo huvurumishwa likiwa limebebwa begani na hivyo ni rahisi kulihamisha. Makombora ya Strela 2 yalikuwa na jukumu kuu katika vita vya Vietnam dhidi ya Jeshi la Marekani na zaidi ya helikopta elfu tatu za Marekani zilitunguliwa kwa makombora hayo ambayo kiasili ni ya Russia.
Baada ya Vita vya Seif al-Quds mwezi Mei 2021, Hizbullah ilizidisha juhudi zake za kutengeneza makombora ya kutungulia ndege ili kupunguza hatari ya ndege za kivita za Israel na hivyo kufanikiwa kupata makombora hayo.
Kwa kutengenezwa makombora hayo, jeshi katili la Israel limeingiwa kiwewe kwani hata wakati wa vita vyake dhidi ya Gaza 2014, wakati majeshi ya wapigania ukombozi wa Palestina yalitumia bunduki za 14.5 mm, helikopta za Israel hazikuthubutu tena kukaribia Gaza.
Kadhia hizo zinaonyesha kuwa, kadri muda unavyosonga mbele, ukiritimba wa anga wa jeshi la utawala haramu wa Israel unasambaratika, na siku baada ya siku vikosi vya muqawama kama vile Hizbullah na Hamas vinaimarisha uwezo wao wa kujihami angani na pia katika medani za nchi kavu na baharini.