Maseneta wa Ufaransa wakosoa sera ya Macron barani Afrika
(last modified Wed, 09 Aug 2023 11:40:26 GMT )
Aug 09, 2023 11:40 UTC
  • Maseneta wa Ufaransa wakosoa sera ya Macron barani Afrika

Maseneta karibu 100 wa Ufaransa wamekosoa vikali sera za Rais Emmanuel Macron wa nchi hiyo barani Afrika na kusisitiza kuwa, sera hizo zimechochea misimamo hasi dhidi ya Ufaransa katika nchi za bara hilo.

Katika barua yao ya wazi kwa Macron iliyochapishwa katika gazeti la Kifaransa la Le Figaro, maseneta hao 94 wamemtaka rais huyo wa Ufaransa aangalie upya sera za serikali yake mkabala wa bara la Afrika.

Maseneta hao wamekiri kuwa, kufeli kwa Operesheni ya Barkhane kulichangia pakubwa kukataliwa Ufaransa katika nchi za Mali, Burkina Faso, Niger na Jamhuri ya Afrika ya Kati. Macron alitangaza kusitisha Operesheni ya Barkhane ya eti kupambana na magenge ya kigaidi katika eneo la Sahel la Afrika mwaka 2021.

Maseneta wa Ufaransa wamesema hivi sasa mataifa hayo ya Afrika Magharibi hayataki kuwa na ushirikiano wa kiuchumi, kisiasa na kijeshi na Ufaransa kutokana na sera mbovu za Macron.

Sehemu moja ya barua hiyo ya maseneta wa Ufaransa kwa Macron inasema: Je huu si wakati wa kuangalia upya mtazamo wetu kwa Afrika na mfungamano baina ya pande mbili?

Wananchi wa Niger na bendera ya Russia katika maandamano dhidi ya Ufaransa

Haya yanajiri siku chache baada ya Gérard Araud, balozi wa zamani wa Ufaransa nchini Marekani, Umoja wa Mataifa na katika utawala haramu wa Israel kusema kuwa, mapinduzi ya kijeshi Niger yanatokana na wananchi kuchoshwa na uingiliaji wa Ufaransa na kukataa kwao uwepo wa dola hilo la Ulaya nchini humo.

Ufaransa ina wanajeshi 1,500 nchini Niger. Maelfu ya wananchi wa Niger hivi karibuni walifanya maandamano katika mji mkuu Niamey, wakitaka kufukuzwa nchini humo mara moja wanajeshi hao wa Ufaransa na wa nchi nyingine za Magharibi.

Wananchi hao wa Niger wanaounga mkono mapinduzi yaliyofanyika karibuni, huku wakitaka Wamagharibi wasiingilie mambo ya ndani ya nchi yao, walipeperusha bendera ya Urusi na kutoa nara na kaulimbiu dhidi ya Ufaransa na Marekani.