Sep 02, 2023 02:43 UTC
  • Kujiunga Jumuiya ya ASEAN na juhudi za kutumia sarafu za kieneo badala ya dola

Kufuatia kutiwa saini makubaliano ya kifedha kati ya Indonesia, Malaysia na Thailand, sarafu za ndani za nchi hizo sasa zitaanza kutumika katika masoko ya biashara ya Jumuiya ya Kusini Mashariki mwa Asia (ASEAN).

Magavana wa benki kuu za Indonesia, Malaysia na Thailand, wakiwa pambizoni mwa kikao cha Mawaziri wa Fedha wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Kusini Mashariki mwa Asia (ASEAN) huko Jakarta, mji mkuu wa Indonesia, wametia saini makubaliano ya kuanza kutumika rasmi na kivitndo sarafu za nchi zao katika mabadilishano ya kibiashara na hivyo kufutilia mbali matumizi ya dola ya Marekani katika masoko ya kibiashara ya jumuiya hiyo. Indonesia ambayo kwa sasa inashikilia uenyekiti wa zamu wa Jumuiya ya Mataifa ya Kusini Mashariki mwa Asia (ASEAN) imeanzisha mfumo wa ushirikiano wa LCT na nchi wanachama wa ASEAN. Mkataba wa LCT ulitiwa saini kati ya nchi kumi wanachama wa Jumuiya ya Nchi za ASEAN na China, Japan na Korea Kusini, kwa ajili ya kupanua ushirikiano wa kifedha wa kieneo.

Moja ya vifungu muhimu vya mkataba huo ni kukuza matumizi ya sarafu za ndani na kupunguza utegemezi kwa dola ya Marekani. Kuhusiana na hilo, Bima Yadhastara, mkurugenzi wa Kituo cha Mafunzo ya Uchumi na Sheria cha Indonesia ambaye pia ni mtaalam mashuhuri wa masuala ya kiuchumi wa nchi hiyo anaamini kuwa uenyekiti wa kiduru wa Jakarta katika Jumuiya ya Mataifa ya Kusini Mashariki mwa Asia ASEAN mwaka huu wa 2023 ni fursa nzuri ya kukuza matumizi ya fedha za kitaifa katika miamala ya kibiashara, ndani ya mfumo wa makubaliano ya LCT. Kabla ya hapo jumuiya nyingine muhimu kama vile Eurasia, Shirika la Ushirikiano la Shanghai na BRICS zimesisitiza azama yao ya kuondoa dola katika miamala ya kibiashara kieneo.

Bendera za nchi wanachama wa ASEAN

Nchi kadhaa za Amerika ya Kusini na Kati pia zimekuwa zikifanya juhudi za kufutilia mbali matumizi ya dola katika miamala yao ya kibiashara. Kupanuliwa ushirikiano na nchi mpya kunatajwa kuwa moja ya mipango muhimu zaidi ya serikali ya Indonesia wakati huu wa uenyekiti wa nchi hiyo katika Jumuiya ya ASEAN. Kwa kuzingatia juhudi maradufu zinazofanywa na nchi tofauti duniani kwa lengo la kuondoa dola ya Marekani katika shughuli za biashara za kieneo, weledi wengi wa mambo wanaamini kwamba kufuatia kusainiwa makubaliano ya hivi karibuni ya kuondoa dola ya Marekani katika mabadilishano ya kibiashara ya kikanda, suala hilo litaimarisha haraka matumizi ya sarafu za kieneo katika mzunguko mpana wa mabadilishano ya biashara ya nchi wanachama wa Jumuiya ya ASEAN.

Wakuu wa nchi 10 wanachama wa Jumuiya ya ASEAN hivi karibuni walizindua mfumo wa malipo ya kielektroniki mpakani kwa kutumia sarafu zao za kieneo. Kwa mujibu wa takwimu zilizochapishwa karibuni na Shirika la Fedha la Kimataifa IMF, kufuatia kupitishwa na nchi nyingi za dunia mipango ya kuondoa dola katika mizunguko ya kifedha, hisa ya dola katika hifadhi za fedha za kigeni ulimwenguni ilipungua kutoka asilimia 71 mwaka 2000 hadi asilimia 58 mwaka uliopita wa 2022. Tafiti zinaonyesha kuwa utekelezaji wa mkakati wa kuondoa dola katika miamala ya kieneo na kimataifa unahitaji mlolongo wa usambazaji fedha kimataifa. Iwapo nchi nyingi zitageukia matumizi ya sarafu za ndani badala ya dola na euro katika biashara zao, bila shaka matokeo chanya ya suala hilo yatazinufaisha nchi wanachama wa jumuiya za kieneo zinazonapinga siasa za kujitanua na za upande mmoja za Marekani, ikiwemo jumuiya ya ASEAN. Machapisho ya takwimu za Shirika la Fedha la Kimataifa pia yanaonyesha kuwa uchumi wa Marekani unakabiliwa na hatari kubwa kutokana na kuondolewa dola katika shughuli za kibiashara za nchi mbalimbali duniani. Ni dhahiri kwamba kuendelea mchakato huo kutasababisha uharibifu wa kimsingi katika uchumi wa Marekani na hivyo kutayarisha mazingira ya kuporomoka uchumi wa nchi hiyo ya kibeberu ulimwenguni.

Tags