HAMAS: US lazima iishawishi Israel ikubali usitishaji vita wa kudumu Gaza
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i112920-hamas_us_lazima_iishawishi_israel_ikubali_usitishaji_vita_wa_kudumu_gaza
Kiongozi mwandamizi wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS amesema Marekani haina budi kuushawishi utawala wa Kizayuni wa Israel ukubali usitishaji vita wa kudumu kama sehemu ya makubaliano ya kumaliza vita vya mauaji ya kimbari vya Israel katika Ukanda wa Gaza.
(last modified 2024-06-14T07:31:10+00:00 )
Jun 14, 2024 07:29 UTC
  • HAMAS: US lazima iishawishi Israel ikubali usitishaji vita wa kudumu Gaza

Kiongozi mwandamizi wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS amesema Marekani haina budi kuushawishi utawala wa Kizayuni wa Israel ukubali usitishaji vita wa kudumu kama sehemu ya makubaliano ya kumaliza vita vya mauaji ya kimbari vya Israel katika Ukanda wa Gaza.

Osama Hamdan, Mwakilishi wa HAMAS nchini Lebanon amesema hayo katika mahojiano na kanali ya televisheni ya CNN na kuongeza kuwa, pendekezo la Israel la kusimamishwa vita hivyo kwa muda halikubaliki.

Hamdan amesema: Waisraeli wanataka usitishaji vita wa wiki sita, kisha waanzishe tena vita; nadhani Wamarekani mpaka sasa hawajaweza kuishawishi Israel ikubali usitishaji vita kamili. Kadhalika Hamdan ameeleza bayana kuwa, hajui idadi kamili ya Wazayuni wanaoshikiliwa kama 'wafungwa wa vita' katika Ukanda wa Gaza.

Hata hivyo ameongeza kuwa, "Shambulio la Israel la kuwakomboa mateka wanne Jumamosi iliyopita lilipelekea kuuawa Waisraeli watatu na Mmarekani mmoja.

Jinai za Israel huko Gaza

Kabla ya hapo, afisa huyo wa ngazi ya juu wa HAMAS alisema Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Anthony Blinken anabeba dhima ya kutofikiwa makubaliano tarajiwa ya kusitisha vita katika Ukanda wa Gaza kutokana na matamshi na misimamo yake.

Aidha amekosoa vikali matamshi ya Blinken kwa kudai kwamba harakati hiyo ya muqawama ndio inakwamisha kufikiwa makubaliano ya usitishaji vita Gaza. Viongozi wa HAMAS wanasisitiza kuwa, kipaumbele chao ni "kusimamishwa kikamilifu" mashambulizi yanayoendelea ya Israel dhidi ya watu wasio na ulinzi wa Ukanda wa Gaza.