Sep 19, 2023 06:45 UTC
  • Taliban yasema itajibu mapigo endapo Pakistan itaishambulia kijeshi Afghanistan

Katika mjibizo kwa kitisho ilichotoa Pakistan cha kufanya mashambulio ya kijeshi ndani ya ardhi ya Afghanistan, msemaji wa serikali ya Taliban amesema Kabul itajibu mapigo kwa shambulizi lolote litakalofanywa.

Anwar Haq Kakar, Waziri Mkuu wa serikali ya mpito ya Pakistan ameituhumu Taliban ya Afghanistan kwamba inayaunga mkono makundi ya kigaidi yanayoipinga serikali ya Islamabad na kusema kuwa Pakistan ina haki ya kujilinda ikiwa mashambulizi yanayofanywa kutokea ardhi ya Afghanistan yataendelea. "Tutachukua hatua zozote zinazohitajika kulinda nchi," Kakar amesema.

Zabihullah Mujahid

Kwa mujibu wa shirika la habari la Tasnim, Zabihullah Mujahid, msemaji wa kundi la Taliban, ametangaza kwamba hakuwa na habari kuhusu onyo lililotolewa na waziri mkuu wa serikali ya mpito ya Pakistan la kufanya operesheni za kijeshi ndani ya ardhi ya Afghanistan na akasisitiza kwa kusema: endapo itachukuliwa hatua yoyote ya kijeshi dhidi ya ardhi ya Afghanistan, serikali ya Kabul itajibu mapigo kwa shambulio hilo.

Mujahid amesema: Nasaha zetu kwa Pakistan ni kutatua masuala yake ndani ya nchi hiyo na kujiepusha na kutoa tuhuma zisizo na msingi.

Pakistan inadai kuwa, kundi la kigaidi la Tehreek-e-Taliban la nchi hiyo linapanga mashambulizi linayofanya dhidi ya eneo la kaskazini mwa nchi hiyo kutokea ndani ya ardhi ya Afghanistan na kwa uungaji mkono wa serikali ya nchi hiyo ya Taliban. Hata hivyo Taliban imekanusha madai hayo.../

 

Tags