Upinzani mkali wa Marekani dhidi ya juhudi za kusitisha vita Ghaza
Marekani ikiwa ni mshirika wa kistratijia wa utawala wa Kizayuni si tu kwamba inatoa misaada ya kila aina ya silaha na fedha kwa ajili ya kuushambuliwa Ukanda wa Ghaza, bali pia inapinga vikali usitishwaji vita katika uvamizi huo wa umwagaji damu kwa visingizio vya uongo na visivyo na msingi.
John Kirby, Mratibu wa Kistratijia wa Mawasiliano katika Baraza la Usalama wa Taifa la Ikulu ya White House, alidai Jumanne kwamba sasa sio wakati mwafaka wa kusitisha mapigano katika Ukanda wa Ghaza. Akisisitiza kwa njia isiyo ya moja kwa moja ulazima wa kuendelezwa mauaji ya watu wa ukanda huo yanayofanywa na utawala wa kigaidi wa Israel, Kirby alidai kuwa Tel Aviv ina haki ya kujilinda na kuwalenga viongozi wa Hamas. Pia aliongeza kuwa Marekani itaendelea kuiunga mkono Israel na kutoa misaada yote inayohitajika kwa utawala huo kwa ajili ya kuendeleza vita dhidi ya watu wa Ghaza.
Msemaji huyo wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani Jumatatu pia alipinga usitishaji vita huko Ghaza na kudai kwamba usitishaji vita wowote utaipa Hamas fursa ya kuimarisha vikosi vyake ili kuendeleza mashambulizi dhidi ya utawala gaidi wa Kizayuni.
Baada ya operesheni ya Kimbunga cha Al-Aqsa ya Hamas na makundi mengine ya muqawama huko Ghaza dhidi ya utawala wa Kizayuni tarehe 7 Oktoba, ambayo ilisababisha vifo vya Wazayuni wasiopungua 1,500 na kujeruhiwa karibu 5,000 kati yao, baraza la mawaziri la Wazayuni liliamuru kuanza mashambulizi makubwa na ya kinyama katika Ukanda wa Ghaza. Kwa mujibu wa takwimu za Wizara ya Afya ya Palestina, idadi ya wahanga wa hujuma hiyo kali ya utawala wa Kizayuni dhidi ya wananchi wa Ukanda wa Ghaza na Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan imefikia zaidi ya mashahidi elfu 5 na takriban elfu 15 kujeruhiwa.
Hivi sasa hali ya Ghaza ni mbaya sana, na utawala wa Kizayuni kwa kuzingatia uungaji mkono wa pande zote wa Washington kwa vitendo vyake vya jinai, badala ya kupunguza vita, umeongeza kwa kiasi kikubwa mashambulizi yake ya mabomu katika maeneo mbalimbali ya Ukanda wa Ghaza.
Hamas ilitangaza Jumatatu katika taarifa kuwa hospitali zote za Ghaza hazina mafuta na kuongeza kuwa msaada ambao umefika katika eneo hilo hadi sasa hautoshi kukidhi mahitaji ya wahanga wakazi wa ukanda huo.
Msimamo wa Marekani kuhusu mashambulizi ya umwagaji damu ya Israel dhidi ya Ukanda wa Ghaza na nafasi yake muhimu katika jinai hiyo si tu kwamba umekabiliwa na ukosoaji mkubwa wa nchi za Kiislamu, bali pia nchi nyingine kama Russia zinaibebesha Washington dhima ya kuendelea hali mbaya inayowakabili hivi sasa watu wa Ghaza.
Sergei Lavrov, Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia alionya Jumatatu kwamba hatua ya Marekani ya kutuma silaha katika eneo la Asia Magharibi inazidisha mizozo katika eneo hilo. Aliongeza kuwa kadiri Marekani inavyozidi kutuma meli za kivita katika eneo Asia Magharibi (Mashariki ya Kati) ndivyo uwezekano wa kuenea mzozo katika eneo hilo unavyozidi kuongezeka.
Marekani hadi sasa imepigia kura ya turufu maazimio mawili yaliyopendekezwa na Russia na Brazil kwa ajili ya kusitisha mapigano ya Ghaza katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na hivyo kuzuia kuidhinishwa kwake. Baraza la Usalama halikuweza kuidhinisha rasimu ya azimio lililopendekezwa na Brazil tarehe 18 Oktoba kutokana na kura hiyo ya turufu ya Marekani. Marekani ilikuwa imedai kuwa rasimu hiyo haikutaja eti haki ya Israel ya kujilinda. Rasimu ya azimio la Russia pia haikutapa uungaji mkono wa kutosha katika Baraza la Usalama.
Nchi tatu za Magharibi, wanachama wa kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, yaani Marekani, Uingereza na Ufaransa, pamoja na Japan, zilipinga azimio hilo. Vasiliy Nebenzia, Mwakilishi wa Kudumu wa Russia katika baraza hilo, alisema kuhusiana na suala hilo kuwa siasa za nchi za Magharibi kwa mara nyingine tena zimeliteka Baraza la Usalama na kulifanya kushindwa kuchukua maamuzi ya pamoja na yenye taathira katika kupunguza mapigano.
Katika hatua ya kuiunga mkono Israel, Marekani imewasilisha rasimu ya azimio ambalo sambamba na kulaani Hamas, inaunga mkono hatua za utawala wa Kizayuni kwa kisingizio cha kujilinda.
Katika asimu hiyo, Marekani imepinga usitishaji vita na ufikishwaji wa misaada ya kibinadamu huko Ghaza, na kulaani operesheni ya Kimbunga cha Al-Aqsa ya Hamas na kuitaja kuwa ni shambulio la kigaidi. Washington vileivle inataka kushinikizwa Hizbullah na makundi mengine ya muqawama ili kukomesha mashambulizi yao dhidi ya Isreal. Kwa kuwasilisha azimio hilo, serikali ya Biden kwa hakika imeonyesha nia yake ya kweli, ambayo ni kuua Wapalestina wengi iwezekanavyo, kwa kupinga usitishaji vita na kuunga mkono hatua zote za Israel zilizo dhidi ya binadamu na za jinai kwa kisingizio tu cha eti kujilinda.
Dmitry Polyansky, Naibu Mwakilishi wa Kudumu wa Russia katika Umoja wa Mataifa, alisema Jumatatu kuwa rasimu ya azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na Marekani kuhusu mzozo wa Palestina na Israel inaibua maswali mengi.