Kremlin: Russia haiwezi kushindwa katika medani ya vita
Msemaji wa Ofisi ya Rais wa Russia (Kremlin) amesema ni muhali kwa jeshi la Russia kushindwa katika medani ya vita.
Dmitry Peskov alisema hayo jana Alkhamisi katika mahojiano na kufafanua kuwa: Wakati umefika kwa kila mtu huko Kiev na Washington kufahamu kuwa, haiwezekani kushindwa jeshi la Russia katika medani ya vita.
Wiki iliyopita, Rais Vladimir Putin alisema serikali za Magharibi zimeanza kupunguza matumaini yao juu ya matokeo ya mgogoro wa Ukraine.
Shirika la habari la Russia Today limemnukuu Dmitry Peskov, Msemaji wa Kremlin akieleza kuwa, vikosi vya jeshi la Russia havipo katika mkwamo au kinamasi kama vilivyo vikosi vya jeshi la Ukraine na waungaji mkono wao wa Magharibi.
Kwa mujibu wa shirika la habari la NBC, maafisa wa nchi za Magharibi wanaendelea kuwa na wasi wasi mkubwa juu ya kuendelea kupungua idadi ya wanajeshi wa Ukraine.
Aidha Wamagharibi, kwa mujibu wa NBC, wana hofu kuwa yumkini watashindwa kuendelea kuimiminia Ukraine silaha, hasa baada ya kuibuka vita vya Palestina na Israel.
Wiki iliyopita, Kamanda Mkuu wa Jeshi la Ukraine, Jenerali Valery Zaluzhny alikiri katika makala iliyochapishwa na gazeti la The Economist kuwa, vikosi vya Kiev huenda visifikie natija yoyote iwapo havitapewa silaha za kisasa na Magharibi.
Msemaji wa Ikulu ya Rais wa Russia ameeleza bayana kuwa, operesheni ya kijeshi ya Russia dhidi ya Ukraine iliyoanza Februari 2022 inahalalishika, ni ya dharura na inapaswa kuendelea hadi tamati.