Nov 21, 2023 07:12 UTC
  • Ukosolewaji mkali wa undumakuwili wa Magharibi kuhusu kadhia ya Israel na Wapalestina

Waziri Mkuu wa Ireland, Leo Varadkar amekosoa vikali undumilakuwili wa nchi za Magharibi na kusema kuwa Umoja wa Ulaya na madola ya Magharibi yanashughulikia masuala yanayohusiana na Israel na Palestina kwa undumilakuwili wa wazi.

Varadkar alisema, linapokuja suala la haki za binadamu, kusiwe na ubaguzi na haki za binadamu zinapaswa kuwa za ulimwengu wote, na akafafanua kwa kusema: Umoja wa Ulaya umechukua mbinu ya kupitisha misimamo yenye vigezo viwili tofauti kuhusu Palestina na Israel.

Aidha ameongeza kwamba: Hii ni pamoja na ukweli kwamba tunaamini kuwa Israel na Palestina zinapaswa kushughulikiwa kwa usawa linapokuja suala la haki za binadamu, na misimamo yetu inalingana na madai yetu katika suala hili, na ndiyo sababu haturuhusu jeshi la Marekani kuondoka kwenye Uwanja wa Ndege wa Shannon au uwanja mwingine wowote wa ndege Ireland kwa ajili ya kuusaidia utawala wa Kizayuni wa Israel.

Maneno hayo ya Waziri Mkuu wa Ireland yamekuja baada ya maelfu ya watu wa nchi hiyo kuandamana katika mji mkuu, Dublin kuunga mkono wananchi wanaoteseka wa Palestina. Waandamanaji hao walikusanyika mbele ya jengo la Wizara ya Mambo ya Nje ya Ireland.

Ukosoaji wa wazi wa mmoja wa wakuu wa nchi za Ulaya juu ya undumakuwili wa nchi za Magharibi, ukiwemo Umoja wa Ulaya, kinara wao akiwa ni Marekani ambayo iko mstari wa mbele kutetea Israel katika jinai zake dhidi  ya Wapalestina kwa mara nyingine tena unadhihirisha undumakuwili wa nchi za Magharibi kuhusu masuala mbalimbali, kuanzia ugaidi na haki za binadamu hadi suala la Palestina.

Kwa hakika serikali za Magharibi huchukua misimamo katika masuala mbalimbali kwa kuzingatia maslahi na malengo yao na huwa hazijali kuhusu kuchukua misimamo inayokinzana na matamko au sera zao za huko nyuma.

Mtazamo huo wa undumakuwuli unadhihirika wazi katika kadhia ya vita vya hivi sasa dhidi ya Ghaza. Kwa mfano watawala wa Marekani na Ulaya wanaeleza masikitiko yao na kulaani vikali operesheni ya wapigania ukombozi wa Palestina ya Kimbunga cha Al-Aqsa kutokana na kuwa walowezi wa Kizayuni waliuawa katika maeneo ya jirani na Gaza. Hii ni katika hali ambayo wengi wao waliuawa katika hujuma ya helikopta ya wanajeshi wa Israel.

Watawala hao wa Magharibi sasa wanapuuza na hata kuunga mkono mauaji ya kimbari ya Wapalestina yanayotekelezwa na utawala wa Israel katika Ukanda wa Ghaza. Watawala hao wa Magharibi hata wanahalalisha vitendo hivyo vya kinyama vya Israel kwa kisingizio cha kanuni ya kujilinda utawala huo pandikizi. Hadi sasa zaidi ya watu 13,000 wameuawa huko Ghaza, kati yao wakiwemo watoto 5,500 na wanawake 3,500. Pia, zaidi ya watu 6,000 hawajulikani waliko katika mashambulizi ya mabomu ya utawala wa Kizayuni, ambapo 4,000 ni wanawake na watoto. Aidha zaidi ya watu 30,000 wamejeruhiwa wakati wa mashambulizi ya utawala wa Kizayuni huko Ghaza.

Idadi hii kubwa ya Wapalestina waliouawa shahidi na kujeruhiwa haikuwasikitisha watawala wa Marekani, Ujerumani, Uingereza na Ufaransa wanaodai kuwa watetezi haki za binadamu. Kwa hakika, uungaji mkono wa kiusalama na kijeshi wa nchi za Magharibi hususan Marekani kwa Israel kwa kisingizio cha kujilinda utawala huo kivitendo ni idhini kwa utawala huo kuwaua kikatili watoto na wanawake wa Kipalestina.

Dmitry Polyansky, naibu mwakilishi wa Russia katika Umoja wa Mataifa anasema: "Vita vya Ghaza vimeonyesha wazi undumakuwili wa nchi za Magharibi, na hata hawathubutu kuyaita matendo ya Israel kama yalivyo (yaani mauaji ya kimbari)."

Maandamano ya waungaji mkono wa Palestina mjini Dublin

Wakati huo huo, baadhi ya misimamo ya kinafiki ya maafisa wakuu wa nchi za Magharibi imesababisha ukosoaji mkubwa dhidi yao. Pamoja na mambo mengine, Ursula von der Leyen, Mkuu wa Kamisheni ya Umoja wa Ulaya, alisisitiza tarehe 6 Novemba katika mkutano wa kila mwaka wa mabalozi wa Umoja wa Ulaya mjini Brussels kwamba Israel ina haki ya kupambana na Hamas. Wakati huo huo, alidai kuwa moyo wake uliumizwa na uharibifu na maafa katika Ukanda wa Ghaza. Maneno yake haya yakawa mada ya mijadala ya watumiaji mitandao ambao walimwita kuwa mwanamke mwongo zaidi barani Ulaya. Watumiaji wa mitandao ya kijamii wanasema kuwa ndiye aliyeipa Israeli idhini ya kuwaua wanawake na watoto wa Ghaza. Claire Daly, mjumbe wa Bunge la Ulaya, aliandika kwenye akaunti yake ya X (Twitter ya zamani) kwamba: Rais wa Tume ya Ulaya Ursula von der Leyen ameipa Israeli mamlaka kamili ya kueneza ukatili na vita kwa kisingizio cha "kujilinda".

Nukta muhimu ni kwamba, tofauti na serikali na viongozi wa nchi za Magharibi wanaounga mkono kikamilifu utawala wa Kizayuni na jinai zake dhidi ya Wapalestina, watu wa kawaida waliowengi katika nchi za Ulaya na Marekani wameandamana dhidi ya mauaji ya kimbari yanayotekelezwa na Israel dhidi ya Wapalestina huko Ghaza huku wakilaani ukimya wa serikali za Magharibi kuhusu jinai hizo.

Tags