Dec 15, 2023 02:56 UTC
  • Kuidhinishwa kuanza rasmi uchunguzi wa kumsaili Biden katika Bunge la Wawakilishi la Marekani

Bunge la wawakilishi la Marekani jana Jumatano lilipasisha azimio kwa kura 221 za ndio mkabala wa 212 za kupinga kuanzisha rasmi uchunguzi wa kumsaili Rais Joe Biden wa nchi hiyo. Kabla ya kura hiyo, Kelly Armstrong, Mwakilishi wa Kongresi ya Marekani kwa niaba ya wajumbe wa Baraza la Wawakilishi la Marekani, alichapisha rasimu ya azimio kwa ajili ya kuendelea uchunguzi huo tajwa kwa lengo la kumuuzulu Rais Joe Biden wa Marekani.

Imeelezwa kuwa kura hiyo si kwa ajili ya kumsaili au kumtosaili Rais wa Marekani, bali ni hatua ya kisheria inayotoa mamlaka zaidi kwa kamati zinazohusika katika uchunguzi. Azimio hilo linavilazimu vyombo vya mahakama na kamati za usimamizi katika Bunge la Wawakilishi kufuatilia na kushughulilia uchunguzi wao wa kesi za tuhuma zinazomkabili Biden na familia yake za kutumia vibaya madaraka na nafasi yao ya kisiasa katika kupokea rushwa.  

Jim Jordan na James Comer, wawakilishi wawili mashuhuri wa chama cha Republican, wameitaja kura ya Baraza la Wawakilishi kuwa ni "ujumbe wa wazi" kwamba raia wengi wa Marekani wanataka kujua chanzo cha mamilioni ya mapato ya familia ya Biden.

Mike Johnson Spika wa Bunge la wawakilishi la Marekani awali alisema kuwa kuna udharura wa kumsaili Biden kwa sababu White House imezuia kufanyika uchunguzi kuhusu tuhuma za ufisadi zinazomkabili kuhusu watu wa karibu yake. Johnson amesema kuhusiana na kuanza rasmi kusailiwa Biden kwamba: Ushahidi unaonyesha kuwa familia ya Biden imepokea mamilioni ya dola kutoka nje. Johnson pia amebainisha kuwa:  Aghalabu ya kamati za masuala ya kisheria zinafanya kazi kubwa katika kutafuta ushahidi wa tuhuma za ufisadi zinazowakabili watu wa familia ya Biden, hata hivyo White House inazuia kutekelezwa mchakato huo huku ikificha maelfu ya kurasa za nyaraka na hati mbalimbali. Kamati tatu za Bunge zinazoongozwa na Warepublican zinamtuhumu Rais Joe Biden kwa kupokea hongo na rushwa wakati alipokuwa Makamu wa Rais wa Marekani. Biden kwa upande wake amepinga tuhuma hizo ambapo kamati hizo za Bunge la Wawakilishi la Marekani hadi sasa zimeshindwa kuwasilisha ushahidi wowote wa kuthibitisha madai yao hayo.  

Joe Biden aliwakosoa Warepublican kwa kile alichokiita "risasi gizani," akisema kuwa: "Warepublican wanalenga kunishambulia kwa kusema uongo na kupoteza muda kwa hila za kisiasa zisizo na msingi."

Wabunge wa chama cha Republican katika Bunge la Wawakilishi wanadai kuwa Biden na familia yake walinufaika kinyume cha sheria na maamuzi ya Biden wakati alipokuwa Makamu wa Rais wa Marekani kuanzia mwaka 2009 hadi 2017. Kamati ya Usimamizi ya bunge hilo pia imedai kuwa familia ya Biden na washirika wake wa kibiashara katika kipindi cha mwaka 2014 hadi 2019 walipokea zaidi ya dola milioni 24 kutoka vyanzo vya fedha huko China, Kazakistan, Romania, Russia na Ukraine. Wabunge wa chama cha Republican wamejikita kufanya uchunguzi kuhusu shughuli za kibiashara anazotuhumiwa kuzifanya Hunter Biden mwana wa kiume wa Joe Biden. Hunter Biden amekaidi matakwa ya Warepubican ya kutoa ushahidi faraghani kuhusu shughuli zake za kibiashara na hivyo kuzidisha hali ya vuta nikuvute kati yake na wabunge wa chama hicho. Warepublican kwa muda sasa wanamtaja na kuamini kuwa Hunter Biden ni sababu kuu ya mgogoro wa kisiasa unaomkabili sasa baba yake. Iwapo wabunge hao wataweza kuzihusisha kwa baba yake shughuli za kibiashara na binafsi za Hunter Biden basi watakuwa wamefanikiwa kutoa pigo kubwa kwa nafasi na kuathiri ushawishi wa Biden miongoni mwa wapiga kura wa Marekani. 

Hunter Biden, anashtakiwa kwa ufisadi

Inaonekana kuwa moja ya malengo ya Warepublican na hasa wafuasi wa Donald Trump rais wa zamani wa Marekani ni kutaka kulipiza kisasi kwa Wademocrat kufuatia kusailiwa mara mbili Trump alipokuwa mamlakani. Wakati huo, Wademocrat walikuwa na wabunge wengi katika Baraza la Wawakilishi  ambapo Nancy Pelosi, Spika wa wakati huo wa Baraza la Wawakilishi ambaye alikuwa akihitilafiana pakubwa na Trump, alikuwa na mchango mkubwa katika kusogeza mbele mchakato wa kumsaili Trump. Wakati huo, Warepublican walitaja kusailiwa Trump kuwa hatua iliyochukuliwa kwa malengo ya kisiasa na kichama khususan kwa madhumuni ya kumdhoofisha Trump katika uchaguzi wa rais wa mwaka 2020 na kulaani hatua hiyo.

Nancy Pelosi, Spika wa zamani wa Bunge la Wawakilishi 

Hivi sasa Wademocrat pia wamedhihirisha msimamo sawa na huo wa Warepublican kuhusu kumsaili Biden; na wanaamini kuwa jitihada zinazofanywa kwa ajili ya kumuondoa madarakani Biden ni wazi kuwa zinatekelezwa kwa lengo la kuchafua jina lake na kupunguza uungaji mkono wa wananchi kwa rais huyo kwa kuzingatia kufanyika uchaguzi wa Rais nchini Marekani mwezi Novemba mwaka ujao wa 2024. Ndio maana wabunge wote wa chama cha Democrat katika Bunge la Wawakilishi la Marekani wakapiga kura ya hapana kwa mchakato wa kuanza kumsaili Biden. Uchunguzi rasmi wa kumuondoa madarakani Biden iwapo utapigiwa kura bungeni na kisha kushtakiwa na Seneti unaweza kuwa tatizo kubwa kwa Biden wakati wa uchaguzi. Bila shaka uchunguzi huu tajwa kama utapelekea Biden kusailiwa na Bunge la Seneti, hautamfanya auzuliwe mamlakani kutokana na wingi wa Wademocrat katika Bunge la Seneti. 

Wakati huo huo kwa kuzingatia masuala mengi ya ndani ya nje yanayoikabili nchi hiyo wananchi wa Marekani wanaamini kuwa kitendo cha Warepublican cha kutaka kumuuzulu mamlakani Biden ni hatua ya kisiasa tu. Wanaona kuwa, wanasiasa wa nchi hiyo katika Kongresi wanatumia muda na pesa za nchi hiyo kwa ajili ya ajenda zao za kisiasa na za vyama ili kumuondoa madarakani hasimu wa upande wa pili badala ya kushughulikia matatizo na changamoto kubwa zinazowakabili. Uchunguzi wa maoni uliofanywa Septemba Mosi mwaka huu umeonyesha kuwa ni karibu asilimia 41 tu ya watu walioshiriki katika uchunguzi huo waliunga mkono wazo la kumsaili Biden ndani ya Kongresi kwa sababu ya kuhusishwa kwake na tuhuma zinazomkabili mwanaye wa kiume Hunter Biden; huku washiriki waliosalia yaani asilimia 35 walipinga jambo hilo, na asilimia 24 pia walisema kuwa bado hawana uhakika kuhusu maoni yao chanya au hasi kuhusu suala hilo.

 

Tags