Jan 02, 2024 02:48 UTC
  • Uchaguzi wa urais wa 2024 na kuongezeka hatari ya ugaidi  ndani ya Marekani

Jena Marie Griswold, Waziri wa Mambo ya Ndani wa Jimbo la Colorado nchini Marekani, amesema kuwa ametishiwa maisha mara kadhaa baada ya kuwasilisha malalamiko yaliyopelekea kuondolewa jina la Donald Trump, mgombea wa chama cha Republican katika uchaguzi wa rais wa Marekani mwaka huu wa 2024 kwenye orodha ya wagombea katika jimbo hilo.

Griswold aliandika katika mtandao wa kijamii wa X siku ya Jumamosi: "Katika wiki tatu zilizopita tangu kuwasilishwa malalamiko haya, nimepokea vitisho 64 vya kuuawa. Baada ya hapo niliacha kuhesabu vitisho." Amesema hatatishika kutokana na vitisho hivyo na kuwa demokrasia na amani vitashinda dhuluma na ghasia. Griswold pia amemsifu Waziri wa Mambo ya Ndani wa Jimbo la Maine, Shana Bellows kwa kuliondoa jina la Trump kwenye orodha ya kura za mchujo katika jimbo hilo na kusema: 'Bellows ni jasiri na shujaa'.

Baada ya kukataliwa ugombea wa Donald Trump,  rais wa zamani na mmoja wa wagombea wa chama cha Republican katika uchaguzi wa rais wa Marekani mwaka 2024 katika jimbo la Colorado na kisha jimbo la Maine, vitisho vya wafuasi wapenda ghasia wa Trump dhidi ya maafisa wa majimbo mawili hayo vimezidi. Mahakama ya Juu ya Jimbo la Colorado wiki mbili zilizopita ilitangaza kwamba Donald Trump hawezi kuwa mgombea wa uchaguzi wa urais wa Marekani katika jimbo hilo kwa kuzingatia Kifungu cha 3 cha kipengee cha 14 cha Katiba ya Marekani. Kifungo hicho ambacho kilipitishwa wakati wa Vita vya ndani nchini humo, kinasema wale wanaokula kiapo cha Katiba ya Marekani watazuiliwa kuchaguliwa tena katika ofisi ya shirikisho ikiwa watachochea ghasia au uasi. Baada ya hapo, Waziri wa Mambo ya Ndani wa Maine, Shenna Bellows, na ambaye anahesabiwa kuwa afisa mkuu wa uchaguzi wa jimbo hilo, alipiga kura ya kupinga Donald Trump kugombea uchaguzi wa rais wa 2024 katika jimbo hilo, akiashiria kipengele cha uchochezi katika katiba. Bellows alisema kuwa Trump  hastahili kushiriki katika uchaguzi huo kutokana na kitendo chake cha Januari 2021 cha kuzusha ghasia katika Bunge la Congress ya nchi hiyo. Alisema wiki iliyopita kwamba walalamikaji katika faili la shambulio la Januari 6, 2021, waliwasilisha ushahidi wa kukinaisha kwa Congress unaothibitisha kuwa wafuasi wa Trump walishambulia na kuibua ghasia katika jengo hilo kwa amri ya Trump na kuwa Katiba ya Marekani inapinga kushambuliwa mihimili ya dola.

Wafuasi wa Trump waliovamia congress

Hata hivyo, uamuzi wa majimbo hayo mawili utatazamwa upya katika Mahakama ya Juu ya Marekani kutokana na rufaa ya Warepublican.

Baada ya kutangazwa maamuzi ya majimbo hayo mawili ya Colorado na Maine ya kutomruhusu Trump kushiriki uchaguzi wa rais, mchakato wa kutishiwa maisha maafisa wa serikali umeongezeka katika majimbo hayo. Kwa hakika mwenendo huo ulianza baada ya uchaguzi wa rais wa Marekani 2020 na kutangazwa mshindi Joe Biden na kushindwa Donald Trump. Trump hakukubali kushindwa na aliwahimiza wafuasi wake kuanzisha uasi na ghasia ili kulalamikia suala hilo. Jambo la kushangaza kuhusiana na suala  hilo ni kushambuliwa Bunge la Congress la Marekani mnamo Januari 6, 2021 na wafuasi wa Donald Trump, ambao wengi wao ni wanachama na waungaji mkono wa makundi yenye siasa kali za mrengo wa kulia. Tukio hilo liliangazia tatizo sugu na kuongezeka ghasia za mirengo yenye itikadi kali pamoja na harakati za ugaidi nchini humo. Alejandro Mayorkas Waziri wa Usalama wa Ndani wa Marekani anasema kuongezeka mirengo yenye itikadi kali ndani ya nchi hiyo ni mojawapo ya vitisho vikubwa vinavyohusiana na harakati za ugaidi nchini humo.

Wagombea wa mrengo wa Repubalican

Rais Joe Biden wa Marekani Januari 2021 aliwaita wafuasi wa Trump wenye silaha kuwa magaidi. Msimamo huo wa Biden unachukuliwa kuwa muhimu sana kwa sababu kiini chake ni utambuzi na uelewa wa asili ya makundi ya kigaidi ya mrengo wa kulia na yenye misimamo mikali ya ubaguzi wa rangi katika nchi hiyo. Inaonekana kwamba nafasi ya makundi yenye misimamo mikali ya mrengo wa kulia imeimarika katika siasa za ndani za Marekani, na kwa kuongeza tofauti za kisiasa na mzozo kati ya vyama viwili vya Republican na Democratic inatarajiwa kwamba makundi hayo yatazusha ghasia na fujo katika kampeni za uchaguzi wa rais wa Marekani katika uga wa kisiasa nchini. Hata hivyo, chanzo cha ugaidi ndani ya Marekani kinarudi nyuma miongo kadhaa, ambapo makundi  na watu binafsi huko Marekani wamehusika na matukio makubwa ya ugaidi nchini humo. Wahusika wakuu wa ugaidi wa ndani nchini Marekani ni watu binafsi na makundi yenye misimamo mikali na ya kihafidhina ya mrengo wa kulia. Makundi hayo ni pamoja na mirengo ya kulia na wafuasi wa serikali za majimbo wanaopinga sera za serikali ya shirikisho hadi makundi ya kibaguzi, kijamii na kidini na watu wenye misimamo mikali ambao wanapinga uhamiaji na kupendelea watu wa ngozi nyeupe.

 

Tags